Na Amon Mtega, Ruvuma.
WAZIRI wa Sheria na Katiba ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Songea Mjini Mkoani Ruvuma Dkt Damas Ndumbaro amegawa vifaa vya Mahakama mtandao vitakavyowezesha wafungwa kusikiliza rufaa zao wakiwa gerezani.
Dkt Ndumbaro akikabidhi vifaa hivyo kwenye gereza la mjini Songea na gereza la Kitai lililopo Wilaya ya Mbinga Mkoani humo amesema kuwa lengo la Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ni kutaka kupunguza adhaa ambazo zimekuwa zikiwakuta wafungwa wakati wa kusikiliza rufaa zao.
Waziri Ndumbaro amefafanua kuwa vifaa hivyo vitasaidia wafungwa kusikiliza rufaa zao kwa njia ya mtandao wakiwa gerezani kwa wakati bila kutumia gharama za kasafiri kwenda kuzifuata Mahakama ziliko.
Kwa upande wao mkuu wa gereza la Kitai mrakibu wa Jeshi la magereza SP Nicodemus Tenga na mkuu wa magereza la Songea kamishina msaidizi wa magereza ACP Godson Mahenge wamesema kuwa vifaa hivyo vimefika kwa muda muafaka kutokana na mlundikano wa rufaa za wafungwa hao.
Naye Mbunge wa Jimbo la Mbinga Vijijini Benaya Kapinga amemshukuru Waziri Ndumbaro kwa kuvigawa vifaa hivyo katika magereza hayo na kuwa madai ya kuchelewa kwa rufaa za wafungwa zitapungua.
Aidha Mbunge Benaya Kapinga amesema kuwa licha ya kupatiwa vifaa hivyo kwenye gereza la Kitai ambalo lipo kwenye Jimbo la Mbinga Vijijini amesema kuwa bado kunachangamoto ya ukosefu wa kituo cha Afya ambacho kingehudumia wafungwa , Wafanyakazi na familia zao pamoja na Wananchi wanaozunguka wamaeneo hayo.
Mwisho.








0 Comments