NA WIIUM PAUL, MOSHI.
Mbunge wa Jimbo la Moshi vijijini Profesa Patrick Ndakidemi ameongozana na Waziri wa Maji Mheshimiwa Juma Aweso kwenye uzinduzi wa Bodi ya 10 ya Bonde la Pangani.
Alipopewa nafasi ya kusalimia katika uzinduzi huo, Mbunge Ndakidemi ameitaka bodi hiyo ifanye kazi ya ziada kwenye kutunza vyanzo vya maji vilivyo mlimani.
"Kuna uharibifu mkubwa sana unaohusisha ukataji miti holela katika vyanzo vya maji kwenye maeneo ya Mito miti ya Mikufi inashambuliwa sana hasana maeneo ya milimani" alisema Prof. Ndakidemi.
Mbunge huyo ameuomba uongozi mpya wa bonde la Pangani ushirikiane na Idara ya Misitu na Maliasili kwenye kudhiti uharibifu unaoendelea na watakaopatikana na hatia za kukata miti wachukuliwe hatua za kisheria.
Akiongea katika uzinduzi huo, Waziri Aweso ameitaka Bodi hiyo kusimamia vizuri matumizi endelevu ya rasilimali za maji zilizopo ndani ya bonde ili maji yawe endelevu kwa vizazi vijavyo.
Waziri alimuagiza mkuu wa bonde la Pangani awajibike kikamilifu kusimamia raslimali za maji kumtaka kushirikisha jamii, viongozi wa Dini na wadau wote kwenye kutunza vyanzo vya maji.
Mwenyekiti wa Bodi mpya Mhandisi Ruth Koya amesema hotuba aliyoitoa Waziri wakati wa uzinduzi wa Bodi hiyo wataichukua kama ni maagizo kwao ya kuyafanyia kazi yote aliyoyaagiza na kuandaa mkakati ya kutunza raslimali maji za bonde la Pangani.
Alimshukuru Waziri kwa kumteua kuiongozi bodi ya Bonde la Pangani.
Mwisho.
0 Comments