NA WILLIUM PAUL, SAME.
MBUNGE wa Jimbo la Same mashariki, Anne Kilango Malecela ameibuka na mbinu mpya ya kuwahamasisha wananchi wa jimbo hilo kushiriki kikamilifu katika zoezi la sensa ya watu na makazi kwa kutumia filamu ya Tanzania Royal Tours.
Mbunge huyo ambaye amekuwa akionyesha filamu hiyo kwa njia ya Sinema katika kata mbalimbali imeonyesha kuwa kivutio kikubwa kwa wananchi wa jimbo hilo ambapo wamepongeza kazi nzuri iliyofanywa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hasani katika kutanga vivutio vya utalii.
Mbunge Anne Kilango alisema kuwa, maendeleo huletwa na sensa kwani serikali hufanya bajeti ya miradi mbalimbali ya maendeleo kulingana na idadi ya wananchi wa eneo husika.
Alisema kuwa, kila mwananchi anawajibu wa kuhakikisha maendeleo ya jimbo la Same masahariki yanasonga mbele kwa kujitokeza kuhesabiwa ili serikali iweze kupata takwimu sahihi za idadi ya watu.
“Agosti 23 mwaka huu ni siku ya Sensa Serikali imeshatimiza majuku yake yanayohitajika katika siku hiyo kilichobaki ni sisi wananchi kuonyesha kuunga mkono kwa kujitokeza kuhesabiwa na kutoa majibu yaliyosahihi kwa maswali tutakayokuwa tukiulizwa” alisema Mbunge Anne Kilango.
Mbunge huyo alisema kuwa, jimbo hilo linauhitaji mkubwa wa barabara zinazopitika muda wote pamoja na uhitaji wa maji hivyo majibu ya matatizo yote yatapatikana kwenye Sensa kwa kujitokeza kwa wingi kuhesabiwa.
Aidha Anne Kilango alitumia nafasi hiyo kumpongeza Rais Samia Suluhu Hasani kwa jinsi alivyotoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo katika jimbo hilo upande wa miundombinu, maji na Sekta ya Afya.
Kwa upande wao, wananchi walipongeza kitendo cha Mbunge huyo kuwafikishia filamu ya Tanzania Royal Tours na kuona jinsi Rais ameweza kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii.
“Mheshimiwa Mbunge wetu tunakushukuru sana leo hii umetufanya sisi wananchi wa kata ya Bombo kuishuhudia filamu yetu ya Tanzania Royal Tours ambayo inatangaza utalii wetu wa ndani tunakupongeza sana” alisema Amina Rashidi mkazi wa kata ya Bombo.
Mpaka sasa sinema hiyo ya Tanzania Royal Tours imeshaonyeshwa katika kata za Miamba, Bombo, Maore huku ikitarajiwa pia kuonyeshwa katika kata ya Kihurio na Vunta.
Mwisho….
0 Comments