Header Ads Widget

KULA MAUA INAVYOWALIZA WAKULIMA WA UFUTA LINDI

NA HADIJA OMARY, MATUKIO DAIMAAPP

Minada ya ufuta tayari imeshafanyika na msimu wa zao hilo kufungwa rasmi. Takwimu rasmi kutoka kwa Ofisa Ushirika Mkoa wa Lindi, Projestus Paschal zinaonyesha kuwa zaidi ya tani 43,000 za ufuta ghafi zimeuzwa katika minada 14 iliyofanyika katika msimu huu wa mwaka 2022/2023.


Mauzo hayo ya ufuta ghafi katika minada iliyofanyika mkoani Lindi, yanatajwa kuwa na thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 134. Yani milioni elfu 134. 


Hizi ni fedha nyingi ambazo zinaweza kujenga barabara ya lami yenye urefu wa zaidi ya kilometa 130 kwa wastani wa kilometa moja kugharimu shilingi bilioni 1. Huu ni ubali wa kutoka jijini Dar es Salam mpaka Kibiti mkoani Pwani. 


Hata hivyo swali la kujiuliza ni hili; katika fedha hizo, ni kiasi gani ambacho kimeingia katika mifuko ya wakulima wa zao hilo ambao kwa hakika ndiyo waliovuja jasho kuanzia kulima mashamba, kupanda, kufanya palizi na kuvuna? 


Jawabu au majawabu ya swali hili yanayopatika kutoka kwa wakulima wenyewe pamoja na baadhi ya wadau ambao wanahusika katika mnyororo mzima wa zao la ufuta, yanatoa taswira inayoonyesha jinsi sura ya mkulima isivyo fika wala kufahamika kwenye minada ya ufuta.



Licha ya kwanza tija katika uzalishaji huonekana kutokana na juhudi kubwa za wakulima kutumia mbinu kadha wa kadha, lakini manufaa ya kubadilisha maisha yao huwa kizungumkuti kutokana na wakulima wengi kuuza mali shambani. Hali hii inachangiwa na mtindo unaoitwa ‘kula maua’. Kula maua ni nini?


KULA MAUA NI NINI?

Ni mfumo wa ununuzi wa ufuta ambao uko katika ngazi ya kutoa maua katika kukua kwake. Ukiwa katika hatua hiyo, wafanyabiashara hutembelea wakulima mashambani kwa lengo la kununua ufuta ambao bado haujakomaa.


Kwahiyo makubabaliano hufanyika baina ya mwenye shamba na mnunuzi wa ufuta, na mara nyingi wakulima ndiyo huwafuata wafanyabishara wakilenga kupata pesa kwa ajili ya kujikimu kwa mahitaji wakati wakisubiri msimu wa mavuno.


Ufuta ukiwa katika hatua ya kutoa mauwa, mnunuzi uenda shambani kwa mkulima ili kufanya tathmini ya ukubwa wa shamba na wingi wa maua, kabla ya kuamua ni kiasi gani cha fedha kinachostahili kutolewa kwa mkulima husika.


Ufuta huo unaonunuliwa kwa mfumo wa kula maua, yaani kabla ya mavuno unanunuliwa kwa shilingi 1,000 (elfu moja) kwa kilo moja.


Baada ya kununuliwa, mfanyabiashara husubiri mpaka mkulima atakapovuna na kuchukua mazao husika bila kuongeza kiasi kingine cha fedha. Tangu anapouziwa maua hadi kuvuna, ufuta hukomaa na kuwa tayari kwa mavumo kati ya mwezi na nusu au miezi miwili.


Baada ya mavuno mnunuzi huchukua ufuta wake kulingana na pesa aliyo mpatia mkulima na yeye hupeleka ufuta huo kwa njia rasmi mnadani kwa mfumo wa stakabadhi ghalani, ambako husubiri kati ya siku saba hadi kumi mpaka kulipwa fedha zake.


BEI YA SOKO 

Katika Minada 14 iliyofanywa na vyama vikuu vya ushirika vya mkoa wa Lindi, bei ya juu ya ufuta ilikuwa shilingi 3,184 na Bei ya chini ilikuwa ni shilingi 2, 955 (au wastani wa shilingi 3000).


Hii ina maana kwamba waliouza ufuta wao kwa njia ya kula maua walipunjika kwa zaidi ya nusu ya thamani halisi ya ufuta katika bei ya soko, hali ambayo ni dhahiri iliwaathiri kimapato wakulima hao. 


Wengi wanaouza ufuta wao katika mfumo wa kula maua huwa ni wanawake wajane na wazee ambapo hata hivyo utafiti unaonyesha kati ya wakulima 10 waliouza ufuta wao kwa njia ya kula Maua 4 kati yao ni wajane wasioweza kumudu kununua chakula na mahitaji menginde kwa ajili ya familia zao.



Mmoja wao ni Halima Ismail (60), mjane na mkazi wa kijiji cha Ruhoma kata ya Rutamba Manispaa ya Lindi. Mama huyu anayeishi kwemye kijumba kidogo cha udongo na mjukuu wake wa miaka mitano (5), hana shuguli wala namna nyingine ya kujiingizia kipato zaidi ya kilimo


Halima anasema kuwa analazimika kuuza ufuta wake kwa njia ya kula maua kutokana na hali ya maisha kuwa ngumu na kukosa chakula katika kipindi cha masika, hivyo pesa aliyoipata hununua chakula kwa ajili ya kula na familia yake.


Mwingine ni Mariamu Juma, mama mwenye watoto watatu ambaye pia anasimulia kwamba pamoja kufahamu kuwa kuuza ufuta kwa mtindo wa mtindo wa ‘kula maua’ ni hasara tofauti kuuza kwenye mnada, lakini analazimika kufanya hivyo kutokana na hali ngumu ya maisha hasa wakati wa masika.


"Baadhi ya wakulima tunalazimika kuuza ufuta katika mfumo wa kula maua ili tuweze kupata pesa ya chakula na matumizi madodo madogo ya nyumbani kama vile mafuta ya taa, vifaa vya shule vya wanafunzi na kadhalika.


Naye Ramadhani Nasoro (65) ambaye ni mkazi wa Nihinu tarafa ya Milolo Kata ya Rutamba, Manispaa ya Lindi, anasema yeye huchukuwa hela ya kula maua ili kupata fedha ya kununulia dawa za shambani pamoja na chakula kinachomwezesha kupata nguvu ya kulima akiwa shambani.


“Pesa hii ni ndogo ila kwa sababu tunaipata wakati ambao hatuna kitu kabisa, sisi wakulima inatusaidia kwa kipindi kile ukiangalia mvua inanyesha kila mtu analalamika hana hela hivyo njia pekee ambayo mimi binafsi ninayoiona ya kunikomboa kipindi hiko cha kifuku (masika) ni kukopa hela kwa mfumo huo,” anasema Nasoro.


Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga ni pamoja na kukiri kufahamu kuwepo kwa biashara ya ‘kula maua’ anasema inachangiwa wakulima wenyewe kutokuweka akiba ya fedha baada ya mauzo ya msimu mmoja, kwa ajili ya maandalizi ya msimu unaofuata.


 “Wakulima wengi wanapouza mazao huwa hawakumbuki kama watakuwa tena na mahitaji ya pembejeo katika msimu unaofuata, na hii sio kwa msimu wa ufuta pekee bali hata kwenye msimu wa korosho,”anasema Ndemanga na kuongeza:


“Inafika wakati wa msimu mwingine hana hela hata ya kununua mbegu ama pembejeo, ndio sasa anajikuta anamtafuta mtu atakaemkopesha ili aweze kupata dawa ya wadudu na pesa kwa ajili ya kulimia, matokeo yake anajibana kwa mtu ili akopeshwe fedha kwa ajili ya kuhudumia shamba lake hivyo badala ya kulipa fedha anatakiwa kulipa ufuta. Hli ni tatizo”.


KAULI ZA WANUNUZI

Juma Omari (siyo jina lake halisi ) mkazi wa Manispaa ya Lindi ambaye ni mmoja wa wafanyabiashara wanaojihusisha na ununuzi wa ufuta wa  ‘kula  maua’ anasema kila mwaka hutenga kati ya shilingi milioni 10 na 15 kwa ajili ya kununua ufuta moja kwa moja kutoka kwa wakulima.


Anasema katika biashara hiyo ambayo hufanywa kwa makubaliano kati yake na mkulima, humuigizia faida hata mara tatu ya kiasi alichowekeza kwa wakulima wa ufuta japo inategemea na hali ya soko iliyopo kwa mwaka husika.


Omari alisema kuwa pamoja na biashara hiyo kufanyika kwa siri baina yake na mkulima husika lakini sasa wakulima wenyewe wamesha jua kuwa yeye ujihusisha na biashara hiyo hivyo muda wa ufuta kutoa maua ukifika wakulima wenyewe uenda kwake na kuhitaji fedha ndipo wanapoingia makubaliano.


Mwingine ni Shabani Athuman (pia jina sio rasmi) ambaye pia hufanya biashara ya kununua ufuta ukiwa shambani kwa mfumo wa ‘kula maua’, anasema katika biashara hiyo zipo changamoto kadhaa ambazo wanakabiliana nazo.


Anataja moja ya changamoto kuwa ni ufuatiliaji wa ufuta kutoka kwa wakulima kipindi cha mavuno kwani mashamba yako mbali mbali na muda wa mavuno huwa ni uleule.


"Wapo wakulima ambao ni waaminifu ambao huleta ufuta kwenye eneo nilalokusanyia kulingana na fedha walizochukua, lakini wapo wengine ambao wanataka mpaka tuanze kufuatiliana huko kwenye mashamba yao," anaeleza.


Shaban anasema wakulima wanaokuwa wasumbufu katika kulipa ufuta wakati wa mavuno unapofika, wanajitoa kwenye uwezekano wa kukopeshwa tena katika msimu unaofuata kwa sababu za kukosa uaminifu.


WANAOFURAHIA MAZAO 

Wakati baadhi ya wakulima wakithibitisha kuuza ufuta wao kwa mfumo usio rasmi na kuendelea kupunjika kutoka kwa wanunuzi, hali ni tofauti kwa wakulima wengine ambao waliuza ufuta wao kwa njia ya stakabadhi ghalani 


Teodesia William ambaye ni mkulima wa ufuta, mkazi wa Wilaya Nachingwea, Lindi aliishukuru Serikali kwa kusimamia vyema uuzwaji wa zao hilo la ufuta ambao umeleta tija kwa wakulima kupata bei mzuri.


“Bei hizi ni mzuri na zinaleta manufaa kwa wakulima kwa sababu ukifanya hesabu kutoa matumizi ya maandalizi ya shamba, pembejeo kulima mpaka kusafirisha kupeleka mnadani bado mkulima anabaki na faida kubwa na tija ya kilimo alichokifanya inaonekana” anasema Teodesia.


Naye Amina Saidi, mkulima na mkazi wa Manispaa ya Lindi, mbali na kuishukuru Serikali kusimamia vyema zao hilo na kuwafanya wakulima kupata bei mzuri aliiomba serikali kutoa pembejeo za ruzuku kwa wakulima wa ufuta ili kuongeza tija ya zao hilo.


Kwa mujibu wa Ofisa ugani wa Kata ya Narung’ombe, wilayani Ruangwa Mkoani Lindi, Idrisa Mpwawa, katika kuandaa shamba la ufuta mkulima hutumia si chini ya shilingi 460,000 kwa hekari moja ya shamba la ufuta.


“Hii inategemea na mkulima endapo kama shamba analolitumia amekodi na vitendea kazi vingine kama vile kamba za kupandia atakuwa hana ndio atatumia kiasi hiko cha fedha lakini endapo shamba litakuwa ni la kwake basi uwezekano wa gharama hizo kupungua unakuwepo,”anasema Mpwawa.


Alisema katika hekari moja ya ufuta mkulima ana uwezo wa kuvuna kati ya kilo 600 hadi 800 japo hutegemea mbegu aliyotumia kupanda kwenye shamba lake.


MWONGOZO WA KUUZA UFUTA

Biashara ya ufuta kwa mfumo wa ‘kula maua’ imekuwa ikifanyika na kushamiri kila mwaka, licha ya kuwapo kwa mwongozo wa ununuzi wa ufuta na mbaazi ambao pia hutolewa na uongozi wa mkoa wa Lindi kila msimu wa zao hilo.


Mwongozo wa msimu wa mwaka 2022/23 umezingatia mfumo rasmi wa stakabadhi ghalani unaosimamiwa na Bodi ya Usimamizi wa stakabadhi za ghala.


Lengo la mwongozo huo unaosimamiwa na Ofisi ya Mrajisi wa Vyama vya Ushirika wa Mkoa wa Lindi, ni kutatua changamoto zilizojitokeza katika misimu iliyopita katika mfumo wa mfumo uliowekwa  wa stakabadhi ghalani na ubora wa mazao.


Ofisa Ushirika wa Mkoa wa Lindi, Projestus Paschal anasema wasimamizi wakuu wanaoguswa moja kwa moja katika myororo wa uuzwaji wa ufuta ni vyama vya ushirika.


Mkoa wa Lindi una vyama vikuu viwili ambavyo ni RUNALI kinachojumuisha wakulima wa wilaya za Ruangwa, Nachingwea na Liwale na Lindi Mwambao kinachowaunganisha wakulima wa Halmashauri za Manispaa ya Lindi na wilaya za Mtama na Kilwa.


Wadau wengine ni vyama vya ushirika (AMCOS) halmashauri, pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa abayo chini yake ipo sekretariet ya mkoa inayojumuisha Ofisa Ushirika na Mrajisi wa Vyama vya Ushirika.


Kaimu Mrajisi wa Mkoa wa Lindi, Secilia Socitenes anataja malengo mengine kuwa ni kutatua changamoto za upatikanaji wa takwimu za mauzo, ongezeko la thamani ya mazao, usafirishaji kwa wanunuzi kutoka kwenye ghala za AMCOS, udogo wa ghala za AMCOS na uadilifu wa baadhi ya wadau na viongozi kwenye AMCOS.


Secilia licha ya kukiri kuwa ofisi yake ndiyo yenye dhamana ya kuhakikisha ufuta wote unaolimwa katika mkoa wa Lindi unauzwa kwa kuzingatia mwongozo uliowekwa wa ununuzi wa mwaka 2022/2023, anasema ni vigumu kutambua mazao yaliyovunwa kwa njia ya kula maua.


“Inakuwa ngumu mimi kama afisa ushirika kujua kama mkulima ameuza zao lake nje ya utaratibu kwa sababu yale yanakuwa makubaliano baina ya mnunuzi na mkulima na pia huyo mnunuzi yule anakwenda kuuza ufuta wake kwenye utaratibu tulioupanga kama Serikali  wa stakabadhi ghalani,”anasema Secilia na kuongeza:


 “Kwetu sisi hakuna kinachopotea kwani takwimu halisi za ufuta uliouzwa, tozo za vyama vya msingi (AMCOS) na vyama vikuu vinaweza kuonekana baada ya mnunuzi kulipia ufuta wake alionunua mnadani, hivyo kutoka pale tunaamini kila mdau amenufaika na bei iliyopo sokoni".


Anasema ofisi yake hadi sasa haijapokea kesi, malalamiko wala mashitaka yoyote kuhusu wakulima kudhulumiwa. “Hii inamaanisha wakulima wenyewe wameamua kukubaliana na wanunuzi hao," anasema Kaimu Mrajisi huyo.


Hata hivyo Secilia anasema mwongozo unaosimamiwa na ofisi yake umeweka utaratibu wa kuwachukulia hatua za kisheria wafanyabiashara na kampuni zinazojihusisha na usafirishaji wa ufuta ambao haujanunuliwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani.


Kwa upande wake karani wa chama cha msingi Tulieni (AMCOS), Mariam Lyoka, anasema katika mchakato wa kupokea ufuta kutoka kwa wakulima ni vigumu kujua nani mkulima na nani mfanyabiashara kutoka miongoni mwa wanapeleka ufuta kwa ajili ya kuuza.


Alisema wakati mwingine wakulima uhama kutoka chama kimoja kwenda kingine kutokana na changamoto mbali mbali, hivyo ni vigumu kutambua kuwa huyu ni mkulima halisi ama si mkulima.


“Mfano mwaka huu nimepokea ufuta mwingi tofauti na miaka iliyopita,  maana yake ni kwamba wapo wakulima wengi ambao sio wanachama wa chama chetu lakini wameleta ufuta wao kuuza kwetu na siwezi kusema moja kwa moja kwamba walioleta ufuta wao kuwa ni hao wafanyabiashara walionunua ufuta kwa njia ya ‘kula maua’, anasisitiza Lyoka.


KAULI YA SERIKALI

Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga anasema ili kumaliza changamoto hiyo, upo umuhimu kwa maofisa ugani kutoa elimu kwa wakulima juu ya kujitambua na kulima kibiashara akitambua mfumo mzima wa shughuli zake.


“Mkulima anapaswa kutambua kiasi cha fedha alichotumia katika kuhudumia shamba na kiasi alichopata baada ya mavuno na hiyo itamfanya kutambau kama amepata faida ama hasara,”anasema Ndemanga.


Kuhusu wanunuzi wa ufuta kwa mtindo wa ‘kula maua’, Ndemanga anasema watu hao nio kangomba kama kangomba wengine wanaowarubuni wakulima ambao wananunua mazao nje ya utaratibu na kwamba wanapaswa kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria 


“Kwa nini umkopeshe pesa alafu umuambie akulipe ufuta? Si akulipe pesa alizokopa, tafsiri hapa unamkopesha shilingi 1,000 (elfu moja) na  yeye anakulipa shilingi 3000 (elfu tatu), maana unampa fedha sh.1000 halafu yeye anakulipa ufuta ambao wewe unakwenda kuuza 3000. Huko ni kumnyonya mkulima jambo ambalo hatuliruhusu,”anasema Ndemanga.


“Kama Serikali nikiri jambo hili tunalifahamu, lakini changamoto tunayoipata katika hili ni ushirikiano kutoka kwa wakulima. Ukisema sasa hivi twende kwa mkulima tukamuulize ni nani huyo ambaye ananunua maua’, hawawezi kukwambia. Lakini kama wangethubutu kutwambia, tungeshughulika nao”.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI