Header Ads Widget

KATIBU MKUU CHONGOLO" SITEGEMEI KUIONA SERIKALI IKIPIGA POROJO WALA IKIKUNJA NNE WAKATI WANANCHI WANAPATA SHIDA"

 




NA WILLIUM PAUL, HAI.


KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi, Daniel Chongolo amesema kuwa, kazi ya Serikali ni kutafuta njia za kutatua matatizo ya wananchi na sio porojo.


Chongolo alitoa kauli hiyo jana alipotembelea ujenzi wa kituo cha Afya na nyumba za watumishi katika kijiji cha Chekimaji kata ya Masama rundugai wilayani Hai mkoani Kilimanjaro ambapo alisema kuwa, kazi ya Serikali ni kutafuta njia ya kutatua changamoto zinazowakabili wananchi na sio vinginevyo.



Alisema kuwa, hawategemei kuona Serikali ikipiga porojo wala ikikunja nne wakati wananchi wanapata shida na pindi wananchi wanapolalamika jukumu la Serikali ni kulitafitia ufumbuzi na hili limeonekana baada ya wanananchi wa kata ya Masama rundugai kuonesha wanauhitaji wa zahanati ambapo walichangisha fedha milioni 11 na kuanza ujenzi Serikali iwaunga mkono kwa kutoa fedha milioni 590.



"Moja ya changamoto ya wananchi ni kulaumu tunasubiria mambo mabaya yatokee tulaumu lakini pale ambapo Serikali na watumishi wake wanapofanya mambo mazuri kulingana na Ilani hatuwapongezi ni lazima tujenge utamaduni wa kupongezana pale tunapoona mambo mazuri" alisema Katibu Mkuu.




Alisema kuwa, tabia ya kusubiri kulaumu na kuchongeana na kutengenezeana nongwa kwenye mabaya tu sio vizuri kwani Binadamu tunakosea.




Akizungumzia changamoto ya barabara ya Bomang'ombe kwenda Rundugai hadi TPC itajengwa kwa kiwango cha lami kwani pia barabara hiyo ni ya mchepuko wa mji wa Moshi hivyo itakapojengwa itarahisisha kupunguza msongamano wa magari kutoka na kwenda Moshi.



"Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hasani katika salamu zake alinihakikisha barabara hii itajengwa na naichukua kwa uzito unaostahili na kila nikimkuta Rais nitakuwa namkumbusha hii barabara" alisema Chongolo.




Aidha Katibu Mkuu huyo amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi Agosti 23 mwaka huu kuhesabiwa kwani sensa ndio maendeleo kwani huduma za jamii zinaletwa kulingana na idadi ya wananchi waliopo eneo husika.



Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Hai, Saashisha Mafue alisema kuwa, wananchi wa kata ya Masama rundugai wanakabiliwa na changamoto ya barabara kutoka Bomang'ombe kwenda Rundugai hadi TPC yenye urefu wa kilomita 25.7.




Mafue alisema kuwa, kutokana na ubovu wa barabara hiyo wakinamama wamekuwa wakijifungilia njiani huku akidai kuwa Barabara hiyo ilitolewa ahadi ya kujengwa kwa kiwango cha lami na hayati Rais John Magufuli na badae Rais Samia naye ameitolea ahadi ya kujengwa na sasa imeshafanyiwa upembuzi yakinifu.



Awali akisoma taarifa ya ujenzi wa kituo hicho, Mkuu wa Divisheni ya huduma za Afya, ustawi wa Jamii na lishe wilaya ya Hai, Dkt. Itikija Msuya alisema kuwa, ujenzi wa kituo hicho pamoja na nyumba ya watumishi utagharimu milioni 629 ambapo Serikali kuu imetoa milioni 590.




Dkt. Msuya alisema kuwa, majengo yatakayojengwa ni jengo la mama na mtoto, jengo la Maabara, umaliziaji wa jengo la wagonjwa wa nje, ujenzi wa miundombinu ya maji safi na maji taka, ujenzi wa nyumba ya watumishi, jengo la upasuaji, jengo la wodi ya Wazazi, na jengo la kufulia.

Mwisho...

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI