Na Amon Mtega,
Songea
KAMPUNI ya Mantra Tanzania Rosatom inayojishughulisha na madini ya Uranium katika Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma imeungana na wakazi wa Songea Mkoani Ruvuma katika mbio za Sensa marathon ambazo zimekuwa rasmi kwa ajili ya kuhamasisha kushiriki Sensa na makazi August 23 mwaka huu.
Akizungumza kuhusu ushiriki wa kampuni hiyo Meneja uhusiano wa mantra Khadija Pallangyo amesema kuwa kampuni hiyo imeshiriki zoezi la kuhamasisha sensa kwa mfumo wa mbio za marathon iliyoandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini Dkt Damas Ndumbaro ambaye pia ni Waziri wa Sheria na Katiba.
Pallangyo amesema kuwa zoezi la Sensa ni jambo la muhimu hivyo kila mmoja anatakiwa kushiriki kikamilifu ili Serikali iweze kuwa na takwimu sahihi za wananchi wake pindi inapopanga bajeti za maendeleo kwenye sekta mbalimbali.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini Dkt Damas Ndumbaro ambaye pia ni Waziri wa Sheria na Katiba aliyeongoza mbio za marathon hizo kwa klometa tano ambazo zilikimbiwa kwenye viunga mbalimbali vya mji wa Songea amesema kuwa lengo la mbio hizo ni kuiunga mkono Serikali kwenye shughuli mbalimbali zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan ikiwemo suala la sensa.
Dkt Ndumbaro amefafanua kuwa Sensa ndiyo inayoweza kutoa taswira sahihi ya muelekeo wa Serikali juu ya kuwahudumia Wananchi katika kutekeleza miradi ya sekta mbalimbali kwa kutumia takwimu sahihi.
Amesema kuwa kama wakazi wa Songea Mjini wakajitokeza kikamilifu kwenye zoezi la Sensa basi itapatikana takwimu sahihi ya muelekeo wa kulipata Jiji la Songea kwa kuwa Jiji huundwa na idadi ya watu,hivyo amewaomba washiriki zoezi hilo kikamilifu.
Aidha Mbunge Ndumbaro amewapongeza kampuni ya Mantra Tanzania Rosatom kwa kushiriki zoezi hilo pamoja na Mbunge wa Vitimaalum kutoka Mkoa wa Ruvuma Mariamu Nyoka ambaye ametoa vifaa mbalimbali vya michezo ikiwemo mipira na jezi kwa timu za mpira wa miguu na mpira wa pete.
0 Comments