Header Ads Widget

TAARIFA MPYA TOKA ACT WAZALENDO

Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo Ndugu Ado Shaibu Ado akiambatana na Katibu wa Fedha na Miradi Rachel Kimambo, Mwenyekiti wa Mkoa wa Dar es salaam Ndugu Renatus Pamba na Mwenyekiti wa Jimbo la Mbagala Ndugu Muhdeen Mkwera amemtembelea na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Wilaya ya Temeke Ndugu Jokate Mwegelo kuhusu masuala mbalimbali ya kimaendeleo.


Akitambulisha malengo ya ziara hiyo, Ndugu Ado amesema amemtembelea Mkuu wa Wilaya ya Temeke kwa ajili ya kubadilishana naye mawazo kuhusu changamoto mbalimbali za Wananchi zilizopatikana kwenye ziara ya Katibu Mkuu kwenye Jimbo la Mbagala kuanzia tarehe 29 Juni 2022 hadi tarehe 06 Julai 2022.


"kaulimbiu ya ACT Wazalendo ni Taifa Kwanza leo na kesho. ACT Wazalendo tumeshakutana na Mh. Rais Samia Suluhu juu ya masuala mbalimbali ya Mwelekeo wa Nchi kisiasa. Leo, nimewaleta viongozi wa Mkoa wa Dar es salaam kuzungumza na Mkuu wa Wilaya ya Temeke. Binafsi ninaamini kuwa tunao wajibu wa kubadilisha siasa za Nchi kwenda kwenye siasa za mkazo wa masuala ya Wananchi. Hili linahitaji ushirikiano wa karibu na viongozi wa Serikali katika kubadilishana mawazo na Taarifa" Alisisitiza Ndugu Ado.


Akijibu hoja zilizoibuliwa, DC Jokate amemshukuru Katibu Mkuu Ado kwa kumtembelea na kuziwasilisha changamoto hizo kwake. DC amemhakikishia  kuwa changamoto zilizowasilishwa kuhusu masuala ya barabara, afya, wamachinga na bodaboda zinaendelea kufanyiwa kazi na Serikali.


"Kuhusu barabara ya Nzasa-Kilungule-Buza, nilifanya mazungumzo na mkandarasi. Ameshalipwa. Ni matumaini yangu kuwa itakamilishwa kwa wakati. Pia, tunatarajia kupata awamu nyingine ya mradi wa DMDP ambao utaneemesha barabara nyingi mlizozilalamikia"-alisisitiza DC Jokate.


Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu Ado Shaibu amemhakikishia DC Jokate kuwa Chama cha ACT Wazalendo kinashiriki na kitaendelea  kushiriki ipasavyo kwenye kuhamasisha Sensa ya Watu na Makazi  kwa sababu ni suala muhimu kwa ustawi wa Taifa letu kiuchumi.


Janeth Rithe, Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano kwa Umma, ACT Wazalendo.

14 Julai 2022.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI