Na Gift Mongi _Moshi
Wanakijiji wa kijiji cha Boro kata ya Kibosho Kirima halmashauri ya Moshi wameazimia kuchangishana shilingi 10000 kwa kila kaya kwa ajili ya kukarabati sehemu korofi za barabara ya Boro eneo la kahawa estate maarufu kama kwa Shah.
Miongoni mwa wanakijiji waliohudhuria mkutano wa kijiji na kutoa maazimio hayo ni mbunge wa jimbo la Moshi vijijini Prof Patrick Ndakidemi ambapo alichangia mifuko 100 ya sementi ikiwa ni kuunga mkono wanakijiji wenzie kwa juhudi wanazozifanya.
Kabla ya mkutano kuanza, viongozi wa kijiji na mbunge walitembelea na kukagua mradi wa ukarabati wa darasa la chekechea katika shule ya msingi Singa Bora ambapo ukarabati ulifanywa kwa nguvu za wana kijiji.
Hata hivyo wanakijiji hao waliweza kupata wasaa wa kusomewa mapato na matumizi kwa mujibu was sheria kanuni na taratibu zinavyoelekeza ambapo mkutano huo ulikuwa umeitishwa na mwenyekiti wa kijiji hicho Laurent Mushi .
"Nashukuru kwa kuikubali ripoti hii ya mapato na matumizi sasa naomba twende katika ajenda nyingine namna ya kumaliza hii kero ya barabara ambapo mara kadhaa imekuwa haipitiki"alisema
Hadi hivi Sasa tayari wanakijiji hao wameshakusanya kiasi cha shilingi laki sita ambapo bado michango inaendelea na kuwa kukamilika kwa kiasi hicho Cha fedha kinachohitajika kutaweza kwenda kutatua kero hiyo ya barabara eneo la Boro
Anna Makoy mkazi wa kijiji hicho alipongeza jitihada ambazo zimefanywa na uongozi wa kijiji kwa kushirikiana na mbunge kwani mambo mengine yanaweza kutekelezeka kwa kuunganisha nguvu kwa pamoja badala ya kuisubiria serikali ifanye kila Jambo
"Huu muamko ni mzuri Sana na sisi kama wananchi tunaungana na mwanakijiji mwenzetu ambaye pia Ni mbunge katika kumaliza hizi changamoto ndogo ndogo badala ya kuisubiria serikali ifanye kila jambo"alisema
Naye Fredrick Mushi alisema suala la maendeleo ni jambo la kila mtu hivyo ni bora serikali iwe inaweka nguvu pindi inapoona wananchi wamejitoa kwa maendeleo kwa kuwaunga mkono.
0 Comments