Header Ads Widget

MAAJABU YA PANYA KUTAMBUA MAJERUHI, WALIOFARIKI AJALINI

 


Na Teddy Kilanga MatukioDaimaAPP,Arusha

Wanasayansi na watafiti wa panya duniani wamegundua na kuwafundisha panya kutambua majeruhi na watu waliopoteza maisha ajalini.

Hayo yamebainika kwenye mkutano unaowashirikisha wanasayansi na watafiti wa panya kutoka nchi zaidi ya 50 duniani ambao wamekutana jijini Arusha kujadili namna ya kuwatumia panya katika udhibiti, ugunduzi wa mabomu pamoja na maambukizi ya ugonjwa wa tauni na uokozi wa majanga ya kidunia.


Katika  mkutano huo wa saba wa kimataifa wa baiolojia ya panya na udhibiti wake, utafiti huo umezidi kuishangaza dunia baada ya kufanikiwa  kuwafundisha panya tisa wa uokozi, kutambua majeruhi na watu waliopoteza maisha katika ajali, hasa kwenye majengo.

 


Mwenyekiti wa mkutano huo, ambaye ni Mtaalamu wa Utafiti wa Ikolojia ya panya kutoka Kituo cha Umahiri cha Utafiti wa panya  Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Profesa Rhodes Makundi, amesema watafiti hao wanaangalia mambo tofauti tofauti.

"Kwanza wanaangalia kitu kinachoitwa taxonomy (utambuzi panya wako wa aina gani), pili biodiversity (katika mazingira wanayoishi, kwamba kuna wanyama gani, wanahusianaje na kingine ni juu ya magonjwa yanayotukabili kutokana na panya.


“Pia tunaangalia udhibiti wa panya, kwa kutumia njia za kiikolojia, tunaangalia tabia za panya, tunaangalia panya wanaopatikana katika milima na mabonde katika Afrika, hasa katika nchi za Afrika ya Mashariki."amesema Profesa Makundi.


Aidha mtafiti huyo amesema jambo lingine wanalilizingatia ni kuangalia matumizi ya panya ili kuleta faida kwa jamii; kwa mfano matumizi ya panya kwenye kugundua mabomu, ugonjwa wa tauni na mambo mengine, ambayo panya anaweza akatumika.


Profesa Makundi, amesema baada ya mkutano huo wanatarajia jopo la wanasayansi hao ambao wamefanya utafiti kwenye nchi tofauti, hususan  kudhibiti panya, wanasayansi wa Tanzania, watajifunza mambo yanayofanyika katika nchi zingine na pale inapowezekana utaalamu huo watauchukua na kuutumia hapa nchini kutatua matatizo ya panya.

 

“Kwa mfano, utafiti wa matumizi ya panya kwenye kugundua kutegua mabomu, kugundua magonjwa ya tauni. unaweza kuona utafiti huo unatumika nchi nyingi kama Cambodia huko."amesema.


Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela, akifungua mkutano huo amesisitiza kuwa

umefika wakati wanasayansi na watafiti kutoka hadharani kuelezea zaidi faida ya eneo hilo ili lisibaki tu kuwa eneo la utafiti.


“Nawaomba sana wanasayansi wetu watoke sasa kueleza faida zake ili jamii ielewe zaidi juu ya faida za hili, kwa sababu tunaona kuna hasara nyingi kwenye upoteaji wa mazao na vyakula."amesema na kuongeza.

 

“...Wataalamu wetu, wanasayansi wetu kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, SUA, ndio ambao wanaendesha kwa kiwango kikubwa mkutano huu. Wanasayansi wengi duniani, ambao wako kwenye eneo hili la kutizama athari na faida za panya, "amesema Mongela.


Mongela amesema mkutano huo ni wa kipekee sana kwani wanatizama athari wanazoweza kusababisha panya pamoja na faida, kwa sababu ni viumbe ambao ni muhimu kwa maendeleo na pia watatizama maeneo yote kimaendeleo, kijamii na kisayansi.


“Wamekuja wanasayansi wabobezi wakubwa wanashiriki hapa, kwa hiyo hili mimi naliona kubwa sana kwa nchi yetu, kwanza kutambulika kwamba tuna kituo cha umahiri lakini, wanasayansi hawa wote wa dunia, kuja kwetu kutambua nafasi ya wanayasansi wetu wa Tanzania na kubadilishana ujuzi na machapisho mbalimbali na kazi za kisayansi za dunia nzima ambazo zinafanyika kwenye eneo hili, hasa utafiti wa panya.”amesema Mongela.


Mtafiti kutoka Shirika la Uhisani la APOPO linalojishughulisha na maisha ya panya, lililopo chini ya SUA, Venance Kiria, amesema shirika hilo limewafundisha panya tisa wa uokozi, ambao mpaka sasa wako kwenye hatua ya mwisho katika ufundishaji.


 “Hivi sasa panya wa Tanzania wana uwezo wa kutafuta mtu akiwa umbali mrefu, lakini si kwa kiwango kile ambacho tunakitaka, na hasa kwenye majengo yaliyopata ajali."amesema Kiria.


Kiria ameongeza hivi sasa kuna ajali nyingi zinatokea kwenye majengo makubwa ya ghorofa kubomoka, kwa hiyo mojawapo ya maafa ni majengo  kubomoka na watu kupoteza maisha na wengine kujeruhiwa, lakini wanashindwa kutoka wakisubiri juhudi zetu ili tuweze kuwaokoa wao.” alisema. 


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI