NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA
Kamati ya Bunge ya Bajeti imeridhishwa na usimamizi wa fedha za UVIKO-19 katika ujenzi wa madarasa,maabara na ofisi katika chuo cha Ufundi Arusha(ATC) maarifu kwa jina la Ufundi Tower ambayo imekamilika kwa asilimia zaidi ya 90.
Akiongea wakati walipotembelea jengo hilo mwenyekiti wa kamati hiyo Daniel Sillo alisema kuwa wamejionea jinsi Fedha za UVIKO-19 zilivyofanya kazi kubwa na kumpongeza Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha vyuo vya ufundi vinakuwa na miundombinu inayokidhi viwango vya utoaji elimu ili kusaidia jamii kuongeza ujuzi na kuleta tija.
Alisema kuwa jengo hilo lililogharimu bilioni 2.2 zimesaidia ujenzi wa madarasa nane yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 880 kwa wakati mmoja,maabara sita zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 270 kwa wakati mmoja ikiwemo ofisi 26 zenye uwezo wa kuchukua watumishi 104.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Elimu, sayansi na teknolojia Omary Kipanga aliishukuru serikali kwa kuboresha vyuo mbalimbali ikiwemo kujenga vyuo vinne vya ufundi katika maeneo ambayo hayakuwa na vyuo ambapo bilioni 20 zimepelekwa kwaajili ya kujenga vyuo vinne katika mikoa ya Rukwa,Geita,Njombe na Simiyu
“ katika chuo hiki Wizara ya Elimu pia imetoa milioni 523 kwaajili ya kununua samani za majengo lakini pia mtaala mpya wa elimu utawezesha na kuwasaidia wanafunzi kupewa ujuzi wa vitu mbalimbali vyenye bunifu zenye tija kwaajili ya kuleta tija kwa wananchi na kuongeza ajira, Alisema
Naye Mkuu wa chuo cha ufundi Arusha Dkt Musa Chacha alishukuru serikali kwa kuhakikisha inaongeza tija kwa vyuo vya ufundi huku akisisitiza kuwa kukamilika kwa jengo hilo kutapunguza msongamano wa wanafunzi katika madarasa na maabara
Alieleza kuwa pia itapunguza msongamano wa wanataaluma katika ofisi chache pamoja na msongamano wa ratiba za masomo kutokana na uchache wa madarasa na maabara ikiwemo kuondoa baadhi ya vipindi kufundishwa muda wa jioni sana na hata nyakati za usiku.
Nao baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo Halima Mdee aliipongeza chuo hicho kwa kuongeza idadi kubwa ya wasichana ambapo katika mwaka wa masomo 2021/22 chuo kina jumla ya wanafunzi 4,693 ikilinganishwa na wanafunzi 2,017 waliokuwepo mwaka 2015/16 ikiwa ni ongezeko la asilimia 132.
0 Comments