Na Hamida Ramadhan,Dodoma
KATIKA kuelekea Sikukuu ya Eid AL-ADHAA, Waislam nchini wameaswa kuchinja wanyama wenye miguu minne.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana mara baada ya sala ya Al jumaa, Shekhe wa Mkoa wa Dodoma, Alhaj Shekhe Mustapha Shabaan amesema mnyama anayetakiwa kuchinjwa katika sikukuu hiyo asiwe mgonjwa wala mwenye ulemavu.
Aidha Shekhe Mustapha amesema mnyama huyo anayetakiwa kuchinjwa kwenye siku hiyo ya Eid Al- Adhaa kwa mujibu wa maandiko ya dini ya Kiislamu ni lazima awe mnyama mwenye aibu ambao ni pamoja na Kondoo, Ngamia, Ng’ombe na Mbuzi.
“Kuchinja siku ya Eid ni sunna na inatakiwa kuchinja baada ya kumaliza sala ya eid kama maandiko yanavyosema kwa wale wenye uwezo wa kuchinja wachinje wanyama wenye miguu minne na wenye aibu wala wasiokuwa na vilema au magonjwa ,”alisema Shekhe Mustapha.
Akielezea kuhusu Sikuu ya Eid Al Adhaa, Shekhe Mustapha alisema ni kwa sababu ya mahujaji kwenda kutekeleza nguzo ya tano ya Kiislamu ya kuhiji Maka.
Katika mkutano huo, kiongozi huyo wa dini pia alikemea vitendo vya ukatili vinavyoendelea nchini ikiwamo unyanyasaji vinavyofanywa na baadhi ya watu kwamba ni kinyume na mafundisho ya Mwenyezi Mungu.
“Kwa sasa yamejitokeza matendo maovu ya ukatili na unyanyasaji jambo ambalo halikubaliki machoni mwa Mwenyezi Mungu na jamii kwa ujumla, ”alisema Alhaji Mustapha.
0 Comments