Na Gabriel Kilamlya NJOMBE
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Njombe mzee Jasely Mwamwala amemuomba Waziri wa nishati January Makambaka kuongeza mkandarasi mwingine wa Wakala wa umeme Vijijini REA kwa kuwa mmoja aliyepata kazi hiyo anazidiwa.
Mzee Mwamwala ametoa kauli hiyo Asubuhi hii wakati Waziri Makamba alipozulu katika ofisi za CCM mkoa na kwamba REA wamekuwa na kasi ndogo ya usambazaji umeme jambo linalosababisha ucheleweshwaji wa usogezaji huduma ya umeme kwa wananchi.
Amesema hata kwenye kijiji alichozindua umeme aliyekuwa Waziri wa nishati kipindi hicho Dokta Medard Kalemani mpaka leo umeme haujasambazwa maeneo yote pamoja na vijiji vingine 20.
Sambamba na hilo lakini pia mwenyekiti huyo amehoji juu ya uwepo wa nguzo za zege zilizosambazwa katika maeneo mbalimbali mkoani Njombe jambo lililozua hofu kwa wananchi juu ya miti wanayolima.
Kwa upande wake Waziri wa nishati January Makambaka amekiri kuwa katika mikoa yenye changamoto katika miradi ya umeme wa REA ni pamoja na mkoa wa Njombe na ndio maana amelazimika kufika kuona ukubwa wa tatizo na namna ya kushughulikia.
Waziri Makamba amesema serikali haiko tayari kuona wanafika mwaka 2024 katika uchaguzi wa serikali za mitaa wakakutana na maswali ya umeme wa REA hivyo ni lazima washughulikie kwa haraka na ukubwa wake.
Juu ya kuongeza mkandarasi wa REA Waziri Makamba amesema hakuna haja ya kuongeza mwingine kwakuwa aliyopo alishasaini mkataba wa kukamilisha kazi hiyo hivyo atakachofanya ni kumsimamia aongeze nguvu kazi.







0 Comments