Na Gift Mongi,Matukio DaimaAPP,
Moshi
Wafanyabiashara wadogo wadogo ambao ni wauzaji wa vipuri vya pikipiki na bajaji mkoani Kilimanjaro wametajwa kuwa miongoni mwa kundi lisilotekeleza wajibu wao wa ulipaji wa kodi kwa wakati na utoaji wa risiti kwa wateja wao.
Ofisa wa mamlaka ya mapato nchini(TRA)katika idara ya elimu kwa mlipa kodi Odupai Papaa akizungumza katika semina iliyoandaliwa na jumuiya ya wafanyabiashara kwa kushirikiana na mamlaka hiyo alisema wafanyabaishara hao bado hawana uelewa wakutosha juu ya ulipaji wa kodi.
"Leo tumekutana hapa kuwasikiliza na tujue kero zenu ili tuone njia sahihi katika kuzipatia ufumbuzi kwani haya ni sehemu ya majukumu yetu tuhakikishe mpo katika mazuri ndipo na sisi tudai Kodi ya serikali"alisema
Kwa mujibu wa Papaa wafanyabiashara hao wamekuwa na kasumba ya kufunga biashara zao na kutoweka pindi maofisa wa TRA wanapokwenda kudai kodi jambo ambalo limeonekana kuwa si sahihi na kuwa mamlaka hiyo si adui kwa wafanyabaishara
"Ni lazima tujenge mahusiano mazuri mfano leo hapa utaona tumeanda semina hii kwa ajili ya kuwasikiliza na kupokea matatizo yanayowakabili ili tuweze kuyatatua na wuweze kufanya biashara zenu kwa amani na kujiongezea kipato"alisema
Alisema kwa hali na mwenendo wa kibiashara ilivyo kama biashara ikiyumba mteja anastahili kuandikia mamlaka hiyo barua na kuinulisha badala ya kubaki akilalamika mitaani pasipokuwa na usuluhisho wa tatizo husika.
Kwa upande wake Tirson Kabuje ambaye ni kaimu meneja wa TRA mkoa wa Kilimanjaro alisema mfanyabaishara anao wajibu wa kutunza kumbukumbu za mauzo sanjari na utoaji risiti jambo ambalo litarahisisha ukadiriaji wa kodi.
Alisema kazi ya watumishi wa TRA ni kuelimisha, kumshauri na kukusanya kodi, hivyo haipaswi mfanyabiashara na ofisa wa TRA kuwa na uadui, na kama kutajitokeza changamoto nyinginezo basi watumie jumuiya za wafanyabiashara katika kupeleka kero ili ziweze kupata utatuzi.
Hilarry Lyatuu ambaye ni mwenyekiti wa jumuiya ya wafanyabiashara mkoa wa Kilimanjaro alisema wao hawana ubishi katika kulipa kodi kwani ni kitendo cha kizalendo bali kinachotakiwa ni serikali kuwaelimisha wafanyabiasha ili waweze kulipa kodi kwa viwango vinavyostahili.
Naye Isack Mlay ambaye ni mfanyabiashara alilalamikia uwepo wa mafundi magari ambao huuza vipuri barabarani kwa bei ya chini zaidi hali inayowapelekea kukabiliana na tatizo la ushushwaji wa bei.
Mwisho.
0 Comments