Header Ads Widget

TUMSAIDIE RAIS SAMIA KUTATUA KERO ZA WANANCHI, SIYO KUWA NA MIGOGORO YA KICHAMA NA KUIWEKA MITANDAONI.



Na.Elisa Shunda, Arusha.

USHAURI umetolewa kwa viongozi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na jumuiya zake jumuiya ya wazazi, uwt na vijana kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan, kutatua changamoto za wananchi na siyo kuwa sehemu ya kuibua migogoro ya kichama na kuiweka mitandaoni.


Hayo yamesemwa leo, na Katibu Mkuu wa Umoja wa Wazazi Tanzania Jumuiya ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Gilbert Kalima, wakati akizungumza katika baraza la wazazi mkoa wa Arusha lililoboreshwa ambapo alisema jukumu la CCM na jumuiya zake ni kuhakikisha serikali wanayoiongoza inawatumikia wananchi wake ipasavyo na siyo kujihusisha na mambo mengine yasiyofaa.



"Jukumu la chama tawala ni kuisimamia serikali kutekeleza na kuwahudumia wananchi wake, sasa wewe kiongozi au mwanachama wa CCM unapojikita kwenye migogoro unategemea nani akusemee kama kuna changamoto mahali husika itaneni katika vikao vya ndani mmalize siyo nje au mitandaoni, kila jumuiya ya chama ina kazi zake katika kuisaidia serikali kutekeleza majukumu yake, mfano sisi wazazi tunajikita kwenye elimu, malezi na mazingira kwa majukumu hayo unapata wapi muda wa kutengeneza migogoro tena mitandaoni;


"Tukiingia katika siasa za mapambano sisi kwa sisi tunadumaza na kufifisha maendeleo ya serikali kwa maana sisi ndiyo wasimamiaji wa ilani ya utekelezaji ya mwaka 2020 hadi 2025, CCM tuwasemee wananchi juu ya changamoto katika biashara zao, barabara, umeme, afya, elimu, maji safi, miundombinu, tusipofanya hivyo wananchi hawatokuwa na imani juu yetu", alisema Kalima.



Aidha katibu mkuu wazazi, Kalima, aliipongeza jumuiya ya wazazi mkoa wa Arusha kwa utulivu walionao katika utekelezaji wa majukumu yao na kiutendaji lakini pia kwa miradi waliyonayo wilaya zote, alisema jumuiya ya wazazi taifa wanapambana kuhakikisha jumuiya hiyo inaimarika kiuchumi kwa kuwa na miradi ya uhakika na kuachana na utegemezi wa shule zake.



"Niwapongeze jumuiya ya wazazi mkoa wa Arusha, mwenyekiti, kamati ya utekelezaji na katibu kwa jitihada kubwa mnayoifanya hadi kuwa na miradi katika wilaya za mkoa wenu, sisi wazazi taifa pia tunapambana kuhakikisha tunakuwa na miradi yetu tofauti na utegemezi wa shule zetu na mwanga umeshaanza kuonekana" alisema Kalima.



Pia katibu mkuu wa jumuiya ya wazazi, ndugu Kalima, alisema viongozi wa kichama kuwa macho wakati huu wa uchaguzi huwa vyama pinzani hutumbukiza wanachama wao kugombea ndani ya chama lengo lao kutuvuruga katika uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 na uchaguzi mkuu 2025 tuwe makini.


Aliongeza kwa kusema uchaguzi wa jumuiya ya wazazi ngazi ya kata ukiisha mikoa yote iandae semina elekezi kwa ajili ya mafunzo ya watendaji, lakini pia akasema jumuiya ya wazazi taifa baada ya uchaguzi wa ngazi ya wilaya, mikoa na taifa wataandaa semina elekezi kwa ajili ya mafunzo hayo lengo kuwapiga msasa watendaji wake wafanye kazi kwa uweledi.


Mwisho

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI