Na Bahati Sonda, Simiyu.
Shirika la umeme (Tanesco) Mkoa wa Simiyu limeanza kutumia mfumo wa kielectroniki wa ni-konekt kupitia komputa na simu za mkononi Ili kurahisisha huduma Kwa wateja wapya pamoja na kupunguza msongamano wa gharama na muda wanapohitaji huduma za kuunganishiwa umeme.
Akizungumza na mafundi umeme wanaotandaza mfumo wa umeme majumbani ofisini kwake mapema leo Meneja wa Tanesco Mkoa huo Alistidia Clemence amesema kuwa mfumo huo utaanza kutumia ifikapo Juni 6, 2022, ambapo wateja watakuwa hawana usumbufu wa kufika ofisi za tanesco watatuma maombi popote walipo.
"Katika Mkoa wa Simiyu tunaenda kuanza utaratibu wa kuomba umeme kwa kutumia njia ya ya kidigitali yaani ni-konekt na kwamba mfumo huu utasaidia kupunguza vishoka kwamba unamfahamu nani Tanesco ndipo uweze kuunganishiwa umeme pamoja na gharama za nauli walizokuwa wanatumia wateja kufika ofisini kuomba umeme" Amesema Clemence
Kwa upande wake mhandisi wa ujenzi Johansen Mukulasi amebainisha kuwa wanachokisisitiza Kwa mafundi ni ufanisi na kuhakikisha wanakidhi vigezo vya usajili kutoka mamlaka ya udhibiti wa huduma za nishati na maji Ili wakidhi kutoa huduma hizo kwa wateja.
Hata hivyo awali mfumo uliotumika ulitaka mteja kutembelea ofisi za Tanesco Ili apate fomu ya maombi kisha aanze kufuatilia usajili na ilichukua siku 30 hadi 90 Ili mteja kuwashiwa umeme hali iliyosababisha wateja kushindwa kupata huduma Kwa wakati.
Kwa upande wao mafundi umeme akiwemo Arnold Musa na Joseph Ikombe wamebainisha kuwa mfumo huo utawarahisishia wao pamoja na wateja wao kuomba umeme kidigitali kwani awali walikuwa wanatumia gharama nyingi na muda mrefu na kwamba mfumo huo utasaidia kuondoa adha mbalimbali walizokuwa wanakabiliana nazo.
0 Comments