Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema amesema ipo haja ya viongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kuendelea kupewa elimu juu ya utoaji taarifa kwa wakaguzi wa hesabu za serikali katika usimamizi wa miradi mbalimbali.
Ameyasema hayo akiwa mgeni rasmi kwenye mkutano maalum wa baraza la madiwani wa Halmashauri hiyo uliolenga kupokea hoja za hesabu za serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2020/2021 ambapo RC Mjema amesema kuna uhitaji wa baadhi ya viongozi wa Halmashaurui hiyo kupewa semina ya utoaji taarifa kwa CAG.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mjema amesema katika kujibu hoja pamoja na utoaji taarifa bado kuna changamoto kwa baadhi ya viongozi kwenye idara mbalimbali hivyo amemsisitiza mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga Jomaary Satura kuandaa utaratibu wa viongozi hao kupata semina.
''Kuna uhitaji mkubwa sana wa kuweza kukaa na menejimenti na wengine kule chini ambao wanatuandikia na kufuatiliza ripoti ili waweze kupata semina maalum ya kuweza kutoa tarifa kwahiyo mkurugenzi panga utaratibu wa kuweza kuwa na semina maalum situ kwenye kujibu hizi hoja lakini kwenye utaratibu pia wa kuweza kujibu yale ambayo yanatakiwa''.amesema RC Mjema
Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko amewaomba viongozi kuhakikisha fedha za Halmashauri zinatumika kwa mpango uliokusudiwa huku akiahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa dhati.
''Tuwapongeze sana Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga na timu nzima mmevuka malengo ya ukusanyaji wa mapato ukilinganisha na Mwaka jana lakini tuendelee kutua wito kwa viongozi wetu wa serikali maana mara nyingi wamekuwa watu wa kumsingizia shetaji siyo kweli ni tamaa zao tu kikubwa wakusanye fedha wapeleke kwenye akaunti yetu wasikae nazo sisi tutaendelea kuwapa ushirikiano wakati wowote ambapo wanapokuwa wanahitaji msaada wa serikali kuu na tuko tayari kuhakikisha kwamba hoja hizi ndogo ndogo zinaisha kabisa'' amesema DC Mboneko
Naye mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali Mkoa wa Shinyanga Anselm Faustine Tairo ameshauri kuwa uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kuongeza jitahada ili kumaliza changamoto zilizopo.
''Ripoti iliyopelekwa kwa mheshimiwa Rais ilikuwa na jumla ya hoja 79 katika hoja hizo 28 zipo kwenye hatua mbalimbali ya utekelezaji lakini kuna hoja 14 ambazo utekelezaji wake bado haujaanza kabisa lakini pia kuna hoja 35 ambazo zimetekelezwa kikamilifu lakini kulikuwa na hoja 2 ambazo zimepitwa na wakati mimi ambacho naweza kuwashauri ni kwamba Halmashauri inatakiwa kuongeza ngumu katika kutekeleza hoja ambazo zimesalia''.
Katibu tawala wa Mkoa wa Shinyanga Zuwena Omary amesema serikali ya Mkoa wa Shinyanga itaendelea kushirikiana na uongozi wa Halmashauri hiyo ili kumaliza hoja zilizopo.
0 Comments