NA HADIJA OMARY ,MATUKIO DAIMAAPP LINDI
LICHA ya kalenda ya Zao la korosho kuwataka wakulima wa Zao hilo kuanza kupuliza mashamba yao lakini bado baadhi ya maafisa ugani Wilayani Nachingwea Mkoani Lindi hawana uelewa wa kutosho juu ya matumizi Sahihi na salama ya viuwatilifu vya Zao hilo.
Hayo yamebainika wakati wa mafunzo ya matumizi sahihi na salama ya viuwatilifu kwa maafisa ugani hao yaliyotolewa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI Naliendele) .
Akizungumza wakati wa Mafunzo hayo Mtafiti kutoka Taasisi hiyo Bobnoel Asenga alisema kuwa miongoni mwa mambo ambayo bado yanawasumbua maafisa ugani hao ni michanganyo ya viuwatilifu vya magonjwa na wadudu wahalibifu wa zao la Korosho.
Alisema bado kuna uwelewa mdogo juu ya kiwango sahihi cha Mchanganyo wa viuwatilifu kwa ajili ya kupambana na changamoto ya magonjwa na wadudu wahalibifu wa zao hilo.
Asenga aliitaja changamoto nyingine kuwa ni namna ya kutambua tatizo husika na njia ama namna ya kutatua tatizo hilo.
“Mfano Afisa ugani anaweza kukutana na Ugonjwa wa Daibek lakini anakuwa anachanganya na ugonjwa wa bright hivyo anachukua kiuwatilifu cha kupambana na ugonjwa anapiga kwenye mashambulizi ya wadudu lakini vile vile anachukua viuwatilifu vya kupambana na wadudu wahalibifu anapiga kwenye ugonjwa” alifafanua Asenga.
Nae Afisa Uhaulishaji wa Teknolojia na mahusiano kutoka Taasisi hiyo Emanuel Mgimiloko alisema kuwa ili kuleta tija ya uzalishaji wa zao hilo maafisa ugani wanapaswa kufahamu kwa usahihi matumizi ya viuwatilifu kwa lengo la kuwafundisha wakulima katika maeneo yao.
hata hivyo mgimiloko aliwasihi maafisa ugani hao kuendelee kupambana katika kutoa Elimu kwa Wakulima juu ya matumizi sahii na salama ya viuwatilifu ili kufikia lengo la Serikali la kuongeza tija ya uzalishaji wa korosho msimu wa mwaka 2022/2023
alisema Serikali ilipoamua kutoa Pembejeo za Ruzuku kwa wakulima wa Korosho hapa Nchini ilikuwa na nia ya kuongeza uzalishaji wa Zao hilo kufikia Tani laki saba (700,000).
kwa upande wake kaimu Afisa kilimo Wilaya ya Nachingwea Issa Himapanda alisema kuwa pamoja na changamoto zilizojitokeza za uelewa mdogo wa matumizi ya viuwatilifu kwa Maafisa Ugani mafunzo hayo ni sehemu sahihi kwao ili kukuza uzalishaji wa zao hilo la Korosho na kwamba kumekuwa na viuwatilifu mbali mbali ambavyo baadhi yake vikiwa ni vipya.
“Tunavyopata viuwatilifu vipya sio vyema sisi kama wataalamu tukaendelea kukariri viuwatilifu vile vya zamani basi ipo haja ya kupitishwa kwenye matumizi sahihi ya viuwatilifu hivyo vipya ili taaluma hiyo tuweze kuifikisha kwa wakulima wetu” alisema Himapanda
0 Comments