Na Gabriel Kilamlya Matukio DaimaAPP NJOMBE
Mkuu wa Wilaya ya Njombe Kissa Kasongwa ametoa muda wa wiki mbili kwa wataalam wa Ardhi Halmashauri ya mji wa Njombe Kwenda kufanya Tathmini ya Idadi ya watu wanaotumia Ardhi yenye mgogoro katika vijiji vya Madobore kata ya Luponde na Kijiji Cha Mtila Kata ya Matola Dhidi ya Shirika la Watawa la Imiliwaha ili aweze kuutatua.
Ardhi hiyo inayogombaniwa na pande hizo mbili Ina Ukubwa wa Ekari 1026 na Linadaiwa kumilikiwa kihalali na Watawa hao ambao wanalalamikiwa na Wananchi kwa muda mrefu sasa.
Mwenyekiti wa Kijiji Cha Madobore Teofily Myamba anasema Eneo Hilo Lilikuwa Mali yao lakini wanashangazwa kuambiwa waombe kwa masista hao jambo ambalo linawatatiza zaidi kauli iliyoungwa mkono na baadhi ya wananchi wake.
Upande wa Watawa hao wakiwakilishwa na Sista Maria Nyika wanasema hatua iliyopo kwa sasa katika kutatua mgogoro huo inaleta matumaini tofauti na mfumo uliokuwa ukitumika na Viongozi wengi wa Wilaya na Mkoa waliopita.
Kaimu mkuu wa Idara ya Ardhi na maliasili Halmashauri ya mji wa Njombe Bwana Emmanuel Luhamba anakiri kuwapo kwa makosa yaliyofanyika katika utoaji Hati ya umiliki wa Eneo Hilo kwa Watawa hao huku akitoa ushauri wa Kwenda kupata suluhu ya Mgogoro huo.
Mkuu wa Wilaya ya Njombe Kissa Kasongwa akiongozana na kamati ya ulinzi na usalama pamoja na wataalam mbalimbali toka Halmashauri baada ya kusikiliza pande zote ametoa maagizo yenye lengo la kutatua mgogoro huo.
Kwa miaka mingi sasa mgogoro huo umekuwa ukisababisha mtifuano na kuleta athari za Kiuchumi na Kurudisha Nyuma Maendeleo ya Pande Zote Mbili.
0 Comments