NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
SERIKALI kupitia Wizara yake ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imefanikiwa kumaliza mvutano uliokuwepo katika halmashauri ya wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro kuhusu eneo ambalo itajengwa hospitali ya wilaya ya Moshi Vijijini.
Mvutano huo ulikuwa umewahusisha baadhi ya madiwani na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Kastori Msigala, ambapo madiwani hao walitaka ijengwe eneo la Koresa, kata ya Kirua Vunjo Kusini na wengine wakitaka ijengwe kata ya Mabogini.
Akitoa uamuzi kuhusiana na mvutano huo jana Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi Innocent Bashungwa, alisema kuwa hospitali hiyo itajengwa eneo la Mabogini kama ilivyopendekezwa na kamati ya fedha ya halmashauri hiyo.
“Kamati iliyokaa Agosti, 2019, ilipendekeza na hatimae kupitisha kuwa hospitali hii ijengwe Mabogini na uamuzi huu umelenga Azimio la kamati ambao kuna nyaraka unadhibitisha uamuzi wa kamati hiyo kuhusiana na mradi huo”, alisema.
Aidha alisema kuwa mbali na kuzingatia uamuzi wa kamati hiyo, pia uamuzi huo umelenga kigezo cha utayari wa kata husika katika uamuzi huo katika kuupokea mrdai huo.
“Nimetembelea maeneo yote ambayo yalikuwa yamependekezwa; kule Koresa bado mchakato wa serikali ya kijiji kukabidhi ardhi kwa halmashauri ya wilaya ulikuwa unaendelea kutokana na sehemu ya eneo kuwa na mazao ya chakula ambayo yalikuwa mashambani”, alisema.
Aliongeza, “Pale tumeepuka mtego wa serikali kuambiwa ya kuwa imeamrisha kung’olewa kwa mazao ya chakula ili kupitisha mradi”.
Alisema kwa upande wao uongozi wa kata ya Mabogini tayari walishakabidhi eneo a zaidi ya ekari 30 kwa ajili ya mradi huo na kwamba tayari ujenzi wa mradi huo ulikuwa ushaanza kutekelezwa.
“Ili kukidhi mahitaji ya pande zote, serikali inaelekeza halmashauri kuanza mchakato wa ujenzi wa kituo cha afya eneo la Koresa punde mazao yakakapoondolewa mashambani na eneo hilo kukabidhiwa halmashauri”, alisema.
Aidha Waziri Bashungwa alitoa rai kwa viongozi wanaowawakilisha wananchi kujenga mshikamano pale linapokuja swala la utekelezaji miradi inayolenga kuwahudumia wananchi.
“Hapa serikali ilishatoa fedha shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali lakini kukatokea mvutano wa eneo ambalo lingejengwa hospitali hiyo; hali hii ilimsononesha Rais Samia Suluhu Hassan haswa ikizingatiwa wananchi ndiyo wanateseka pale miradi inapochelewa kutekelezwa”, alisema.
Kufuatia uamuzi huo, Waziri Bashungwa aliuagiza uongozi wa Tarura mkoani Kilimanjaro kuanza mara moja mchakato wa kutengeneza miundombinu ya barabara inayoelekea kwenye mradi huo wa hospitali ili iwe tayari kwa ajili ya huduma nyeti zitakazotolewa na hospitali hiyo itakapokamilika ujenzi wake.
Awali akiwasilisha taarifa yake, Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Kastori Msigala, alisema ujenzi wa hospitali hiyo umelenga kusogeza karibu huduma kwa wananchi wa ukanda wa chini tambarare ambao alisema una uhaba wa taasisi za kutolea huduma za afya.
“Asilimia 86 ya taasisi zote za umma na za kibinafsi zinazotoa huduma za afya wilaya ya Moshi Vijijini ziko Ukanda wa juu ambako kulikuwa kuna pendekezo la kujengwa hospitali hii, wakati ukanda wa Kusini Tambarare ambako itajengwa vituop hivyo ni asilimia 14 tu”, alisema.
Kwa upande wake Mbunge wa Moshi Vijijini Prof Patrick Ndakidemi, amesema ujenzi wa hospitali hiyo utakuwa mkombozi kwa wananchi wa ukanda wa tambarare ambao alisema inabidi wasafiri zaidi ya kilomita 40 kufuata huduma muhimu za afya katika hospitali ya rufaa ya Mkoa iliyoko Moshi Mjini.
MWISHO
0 Comments