Na Mwandishi Wetu
BIHARAMULO
WANANCHI katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Kagera wametakiwa kutowaona polisi kata na wakaguzi kata kama maadui na badala yake wawape ushirikiano wa kutosha ili kukomesha vitendo vya kihalifu.
Kauli hiyo imetolewa na Kamishna wa Kamisheni ya Ushirikishwaji wa Jamii Tanzania Dk. Mussa Ali Mussa, wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara ambao umewahusisha wananchi, wenyeviti wa vitongoji na kijiji cha Nyakanazi, uliofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Nyakanazi wilayani Biharamulo.
Dk. Mussa amesema kuwa polisi hao wanapelekwa katika maeneo yao ili kushirikiana nao kuleta maendeleo ya wananchi kwa kutatua changamoto zilizoko katika jamii, ikiwamo kukomesha uhalifu.
Kamishna huyo amewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali ili kujipatia kipato halali, badala ya kuendekeza uvivu ambao matokeo yake unaweza kusababisha kujiingiza katika vitendo vya kihalifu.
Akiwa katika manispaa ya Bukoba kamishna huyo alifanya kikao na wenyeviti wa mitaa, vijiji na kata kutoka katika wilaya ya Bukoba, na kudai kuwa mkoa wa Kagera bado una kiwango kikubwa cha uhalifu ikiwamo mauaji, ulawiti na ubakaji, ambao unahitaji nguvu ya pamoja kukabiliana nao.
Amesema kuwa katika kipindi cha miezi mitatu ya kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu, yametokea wastani wa mauaji kati ya 30 hadi 40 na kwamba idadi hiyo bado ni kubwa.
0 Comments