Baadhi ya waandishi wa habari wakiwa kwenye picha ya pamoja na meza kuu wakati wa sherehe za maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari.
Na Editha Karlo, MatukioDaimaAPP Kigoma
MKUU wa Mkoa wa Kigoma Mhe.Thobias Andengenye amewapongeza wanahabari wa Mkoa wa Kigoma kwa kazi nzuri wanayofanya ya kuhabarisha umma na kuutangaza Mkoa wa Kigoma kupitia kalamu zao.
Hayo ameyasema jana wakati sherehe za maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari,ambapo maadhimisho hayo yamefanyika jana Mei 16 katika ukumbi wa Kigoma social hall ambayo yalihudhuliwa na wageni mbalimbali pamoja na wadau wa habari.
‘’Niwapongeze ndugu zangu wanahabari wa Mkoa wa Kigoma mnafanya kazi nzuri ya kuhabarisha umma sambamba na kuutangaza Mkoa wetu wa Kigoma,kila siku hakuna chombo cha habari kinachokosa habari ya kutoka Mkoa Mkoani kwetu,endeleeni kuhabarisha umma juu ya mambo mazuri yanayofanywa na serikali yetu ya awamu ya sita mkoani kwetu na hata Kitaifa’’Alisema Mkuu wa Mkoa
Aliwataka waandishi wa habari wanapokuwa wanatekeleza majukumu yao ya kikazi wazingatie weledi wa kazi zao,maadili na sheria na taratibu za nchi ili kuepuka kuandika habari ambazo zinakosa uwiano.
Amewataka pia wanahabari kuhamasisha wananchi kujitokeza katika zoezi la kuhesabiwa la sensa ya watu na makazi ambalo litafanyika Agust 23 mwaka huu nchi nzima.
Akisoma hotuba yake kwenye maadhimisho hayo Rais wa umoja wa vyama vya waandishi wa habari Tanzania(UTPC)Deogratius Nsokolo alisema kuwa viongozi wote wa serikali ya Mkoa na taasisi mbalimbali wanatakiwa kutoa ushirikiano kwa wanahabari pale wanapohitajika kufanya hivyo hii itasaidia kuutangaza Mkoa fursa zake pamoja na mazuri yanayofanywa na serikali ya awamu ya sita katika Mkoa wa Kigoma.
‘’Niwaombe wadau wetu wa habari kutumia vyombo vya habari vilivyopo Mkoani kwetu kutangaza mazuri na fursa mbalimbali siyo hadi tusubiri ziara za viongozi wa Kitaifa’’Alisema .
Makamu Mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari wa Mkoa wa Kigoma(KGPC)Jacob Ruvilo wakati akitoa mada yake ameipongeza serikali ya awamu ya sita tangu iingie madarakani mabadiliko katika sekta ya habari yanaonekana kwani yanaenda kwa kasi.
‘’Tumeona serikali yetu imefungulia vyombo vya habari ambavyo vilikuwa vimefungiwa na kuvitaka vifanye kazi kwa kufuata sheria na miongozo ya nchi,pia imetaka sheria za habari ambazo zinalalamikiwa kuminya uhuru wa habari zirekebishwe kwa kushirikiana ha wadau wote tunaipongeza serikali ya awamu ya sita kwa hilo’’Alisema Ruvilo.
Maadhimisho ya uhuru wa vyombo vya habari ufanyika kila mwaka Mei 3 ambapo mwaka huu yalifanyika jijini Arusha na mgeni Rasmi alikuwa Rais wa Jamuhuri wa muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan yakiwa na kauli mbiu isemayo uandishi wa habari na changamoto za kidigitali.
0 Comments