Na Gabriel Kilamlya NJOMBE
Wakati Tanzania ikiungana kuadhimisha siku ya Familia Duniani Mkuu wa Mkoa wa Njombe Waziri Kindamba amewataka wanafamilia kujiwekea utaratibu wa kutenga siku ya kufanya majadiliano ndani ya familia na namna ya kusuluhisha migogoro mbalimbali inayozikabili Familia nyingi na kuipatia majawabu.
Mbele ya Vyombo vya Habari Waziri Kindamba anasema kwa kufanya majadiliano katika familia inasaidia kusuluhisha baadhi ya changamoto huku ripoti za jeshi la Polisi kitengo cha Dawati la Jinsia zikieleza kuwapo kwa matukio mbalimbali ya ukatili unaotokea ndani ya familia.
Elice Simonile ni Afisa Maendeleo ya Jamii mkoa wa Njombe ambaye anasema Serikali imeweka mpango mkakati wa Kitaifa wa kutokomeza ukatili wa Wanawake na Watoto unaoendelea kuwa kikwazo katika Ustawi wa Jamii.
Baadhi ya wananchi na wanafamilia mkoani Njombe akiwemo Neemababy Jelico wanasema upo umuhimu mkubwa wa kuendelea kutolewa kwa elimu ya namna ya familia zinavyopaswa kusuluhisha matatizo yao yanayosababisha mifarakano ndani ya ndoa huku Subiraga Mwaigwisa Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Njombe akisema matukio yaliyokithiri mkoani hapa ni utelekezaji wa Familia.
0 Comments