Header Ads Widget

RAIS SAMIA MGENI RASMI SHEREHE YA MUUNGANO WA NZAZIBAR DODOMA

 


Na Hamida Ramadhan Matukio Daima APP Dodoma

RAIS Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya sherehe ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambayo kitaifa itafanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Aprili 26 mwaka huu.



Akizungumza na wandishi wa habari jana Jijini hapa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Bunge na Uratibu George Simbachawene amesema Kamati ya Maandalizi ya Sherehe hizo ngazi ya wataalam na ngazi ya watendaji wakuu kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Mkoa wa Dodoma inaendelea kukamilisha maandalizi ya kufanikisha sherehe hizo.


“Kama mnavyo fahamu Maandalizi ya Sherehe za Miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yanaendelea vyema Sherehe hizi Kitaifa zitafanyika Aprili 26 mwaka huu  katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, Dodoma  ambapo Mgeni Rasmi atakuwa Rais  Samia Suluhu Hassan,”amesema. 


Simbachawene amesema sherehe hizo zitafanyika kwa uzinduzi wa andiko la Historia ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kongamano litakalowashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo Viongozi waliopo madarakani na Wastaafu, Wanasiasa mbalimbali, Wanazuoni na Wanafunzi wa Vyuo Vikuu pamoja na Wananchi mbalimbali watakaoalikwa kushiriki Kongamano hilo kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.


Amesema sherehe hizo kutakuwa na wageni waalikwa watakaoshiriki kwenye shughuli za kuanzia wiki hili la muungano mpaka kilele ambapo miongoni mwao ni Viongozi wakuu wa Kitaifa wastaafu; viongozi wa Bunge na Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Viongozi wa mahakama, Viongozi wengine wa Serikali, viongozi wa Vyama vya Siasa na Vyama vya Wafanyakazi, Wanafunzi wa Sekondari za Mkoa wa Dodoma

Kamati kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI imeandaa Mashindano ya Insha kwa wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari nchi nzima Mashindano haya yanafanyika kuanzia ngazi ya Shule hadi Mkoa ambapo hadi sasa yamefikia ngazi ya Mikoa na tarehe 23 Aprili, 2022 watapatikana washindi Sita katika ngazi za Taifa kwa idadi ya Washindi Watatu kutoka Tanzania Bara na Washindi Watatu kutoka Zanzibar.


“Kamati ya wataalamu imeomba ridhaa kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa  ya Maadhimisho na Sherehe Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuwa Mikoa, Taasisi za Serikali na Vyombo vyote vya Ulinzi na Usalama viadhimishe Maadhimisho haya kwa kufanya shughuli za Kijamii katika maeneo yao ya karibu au Vikosi na Kambi zao kama vile kufanya usafi, kupanda Miti na kutoa huduma za afya Kitendo hiki adhimu kitaleta hamasa kubwa, Umoja na mshikamano na kuuenzi Muungano wetu kwa heshima na taadhima kubwa,”amesema 



Kwa Upande Wake Waziri Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia muungano na mazingira Selemani Jafo alisema kwa mujibu wa Sensa za Watu na Makazi zilizofanyika Tanzania zinaonyesha kuwepo kwa ongezeko la idadi ya watu.


Amesema Sensa za mwaka 1967 na 2012 inaonyesha mwenendo wa idadi ya watu Tanzania, mwaka 1967 ilikuwa milioni 12.3 na mwaka 2012 ilikuwa milioni 44.9. Kwa mwenendo huo idadi ya watu Tanzania iliongezeka kwa takribani watu 32,615,454 sawa na asilimia 264.9. 


Dkt Jafo amesema inakiwisiwa kuwa, kwa mwaka 2021 idadi ya watu Tanzania ni milioni 59.4. Takwimu hizi, zinabainisha kuwa, sehemu kubwa ya Wananchi wa pande zote za Muungano wamezaliwa baada ya Muungano, hali inayoonesha wazi uwepo wa umuhimu wa utoaji wa elimu ya historia ya Muungano pamoja na masuala ya msingi yanayohusu Muungano. 


“Kutokana na hali hii Ofisi ya Makamu wa Rais iliona umuhimu wa kuandaa Andiko kuhusu Historia,Misingi na Maendeleo ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambalo litatumika kuelimisha umma ambalo litazinduliwa  Aprili 26  siku ya kilele cha Maadhimisho ya miaka 58 ya Muungano. 


Ameongeza kuwa“Baada ya uzinduzi, Ofisi imepanga kuwa na mpango endelevu wa kutoa elimu kwa umma kuhusu historia ya Muungano na masuala ya msingi kuhusu Muungano Inatarajiwa kuwa, Mpango wa elimu kwa umma utaongeza uelewa wa historia ya Muungano na masuala mengine muhimu kuhusu Muungano,”amesema


Naye Waziri was nchi ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi Hamza Hassan Juma amesema kwa upande wa Zanzibar maonyesho yatazinduliwa aprili 24 mwaka huu na makamu wa Rais Dk Philip Mpango na kuhitimishwa Mei 5 mwaka huu.


Ametoa Rai kwa wananchi wa Tanzania Bara na Zanzibar  kujitokeza kwa wingi kushiriki katika maonyesho hayo ili kupata elimu na fursa mbalimbali.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI