Na Hamida Ramadhan Matukio Daima APP Dodoma
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimeti na Utumishi wa Umma na Utawala Bora Jenista Mhagama amesema Serikali Mtandao siyo teknolojia kama inavyochukuliwa na wengi, bali ni matumizi ya TEHAMA katika kuboresha utendaji kazi wa kila siku katika Taasisi za Umma pamoja kutoa huduma kwa Umma.
Hayo ameyasema leo Jijini hapa katika kikao kazi cha wakuu wa Idara za Tehama kujadili uzingatiaji wa sheria Kanuni taratibu viwango na miongozo ya Serikali Mtandao katika Taasisi za umma
Amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025, Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/22 - 2025/26) na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020 kwa pamoja zinatambua nafasi ya TEHAMA katika kufikia malengo ya Taifa na hivyo kusisitiza haja ya ongezeko la matumizi yake katika utendaji wa shughuli za Serikali na utoaji huduma kwa Umma.
"ili kuhakikisha TEHAMA inatoa mchango chanya katika uendeshaji na usimamizi wa majukumu ya Serikali, jitihada mbalimbali zimefanyika na mafanikio yamepatikana katika maeneo ya Sera, Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo; Usimamizi; Miundombinu; Mifumo tumizi na Shirikishi; na Huduma za Serikali Mtandao.
Amesema yameonekana manufaa ya kusanifu, kutengeneza, kusimika na kuendesha mifumo mhimili na tumizi ya kimkakati na kisekta kwa kutumia wataalamu wa ndani kutoka katika taasisi zenu na wataalamu kutoka Mamlaka ya Serikali Mtandao.
Aidha amesema pamoja na mafanikio yaliyopatikana , lakini eneo hilo bado linakabiliwa na changamoto kadhaa za kiutekelezaji, zikiwemo: Kutoshabihiana kati ya taratibu za utendaji kazi Serikalini na teknolojia inayotumika; Kutopatikana thamani halisi ya fedha zinazotumika kwenye miradi ya TEHAMA Serikalini; Kuwepo kwa mifumo isiyowasiliana au kubadilishana taarifa (ndani ya taasisi, na kati ya taasisi na taasisi); Urudufu wa mifumo miongoni mwa Taasisi za Serikali yenye viwango na gharama tofauti zisizo na uhalisia; Huduma za Serikali Mtandao (e-services) kutowafikia wananchi wote hasa wa vijijini; na Kuongezeka kwa matishio ya usalama wa taarifa katika mifumo na Miundombinu ya TEHAMA.
Hata hivyo, amesema uwezo wa kutatua changamoto hizo upo ndani ya taasisi za watendaji hao .
"Hivyo naelekeza yaanze kufanyiwa kazi haraka ikiwemo kuhakikisha Sheria, Kanuni, Viwango, na Miongozo ya Serikali Mtandao inazingatiwa na kufuatwa. "Amesema Mhagama
Awali akiongea kwenye mkutano huo Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao Mhandisi Benedict Ndomba amesema dhana ya Serikali Mtandao, ni matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika utendaji kazi Serikalini na utoaji wa huduma kwa umma.
Ameeleza Lengo la TEHAMA ni kuongeza tija na ufanisi katika utendaji kazi ili wananchi wapate huduma za Serikali kwa urahisi, haraka na kwa gharama nafuu.
"Pamoja na Jitihada hizi, kumekuwepo na baadhi ya Taasisi za Umma zisizozingatia Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao inayoelekeza matumizi sahihi na salama ya TEHAMA, hivyo kusababisha kuwepo kwa urudufu wa Mifumo, Mifumo isiyozungumza na Miradi ya TEHAMA ambayo haijaidhinishwa na Mamlaka hali inayoweza kupelekea Serikali kutopata tija kwenye uwekezaji unaofanyika kwenye TEHAMA," amesema Mkurugenzi Ndomba.
Aidha, amesema ipo pia changamoto ya upungufu wa watalaamu wa TEHAMA wenye uwezo na ujuzi wa kutosha, na uratibu hafifu wa shughuli za TEHAMA ndani ya Sekta mbalimbali na ndani ya Taasisi za Serikali.
Aidha katika kukabiliana na changamoto hizo, Mamlaka imeendelea kuhimiza uzingatiaji wa Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao katika Taasisi za Umma.
Hii ni pamoja na kufanya kaguzi za Mifumo, kufuatilia Usalama wa mtandao na kushughulikia viashiria vya Matishio ya Kiusalama Mtandaoni, kutoa msaada wa kiufundi na kufanya utafiti na Mafunzo kuhusu Serikali Mtandao,"amesema
Aidha, Mamlaka imeendelea kusimamia na kuendesha Miundombinu na Mifumo Shirikishi ya TEHAMA. Aidha, Mamlaka imeandaa mpango kazi kwa ajili ya Mifumo yote ya TEHAMA Serikalini kuweza kubadilishana Taarifa kupitia Mfumo wa GovESB.
0 Comments