Diana Bundala maarufu kama 'Mfalme Zumaridi' na wafuasi wake 83 leo Aprili 14, 2022 wamefikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Mwanza kwa ajili ya mashtaka yanayowakabili.
Mashtaka hayo ni Usafirishaji haramu wa binadamu linalomkabili mfalme Zumaridi peke yake, kushambulia na kuzuia maofisa wa serikali kutimiza wajibu wao linalomkabili mhubiri huyo na wenzake nane na kufanya kusanyiko lisilo na kibali ambalo linamkabili mhubiri huyo na wenzake 83.
Baada ya kufikishwa ndani ya chumba cha mahakama, wakili wa Serikali Mwandamizi, Emmanuel Luvinga amesema upelelezi wa shtaka namba 10 linalomkabili Mfalme Zumaridi peke yake haujakamilika huku akiiomba mahakama hiyo kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya shauri hilo kutajwa.
Kuhusu shtaka namba 11 linalomkabili Mfalme Zumaridi na wenzake nane na shtaka namba 12 ambalo linamkabili mhubiri huyo na wenzake 83, wakili huyo amesema Upelelezi umekamilika huku akiiomba mahakama hiyo kupanga tarehe kwa ajili ya kuwasomea washtakiwa hao maelezo ya awali.
Baada ya kutolewa maelezo hayo, Wakili msomi wa utetezi, Erick Mutta amewasilisha maombi ya dhamana ya washtakiwa wawili ambao ni mshtakiwa namba 18 (Dorcas Marwa) na mshtakiwa namba 38 (Maria Joseph).
Baada ya maombi hayo kuwasilishwa mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Stella Kiama washtakiwa wameachiwa kwa dhamana baada ya kukidhi masharti ya dhamana hiyo ambayo ni kusaini bondi ya maneno ya Sh2 milioni, nakala moja ya kitambulisho na barua ya utambulisho kutoka kwa Mwenyekiti wa serikali ya mtaa.
Kudhaminiwa washtakiwa hao kunamfanya Mfalme Zumaridi kuendelea kusota rumande na waumini wake watano wanaotaka kuendelea kusota naye huku 78 wakiwa nje kwa dhamana.
Shauri hilo limeahirishwa hadi Aprili 28 mwaka huu litakapoitwa kwa ajili ya kutajwa kesi namba 10, na kusoma maelezo ya awali ya kesi namba 11 na 12.







0 Comments