Header Ads Widget

MATUKIO DAIMA MEDIA YASHINDA TUZO YA TMDA

Mwandishi wa Matukio Daima Media mkoa wa Dar es Salaam Andrew Chele akikabudhiwa tuzo ya TMDA 

Na MatukioDaimaAPP, Mbeya.

MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), imetoa tuzo maalumu za kihistoria kwa Waandishi 5  wa Habari kuhusu Udhibiti wa dawa, Vifaa tiba, Vitenganishi na bidhaa za tumbaku kwa mwaka 2021-2022.


Miongoni mwa waliopata tuzo hiyo ni pamoja na Mwakilishi wa mtandao  wa MATUKIO DAIMA MEDIA, Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Andrew Chale.


Washindi wengine wa tuzo hizo ni Bw. Waziri Suca kutokea Tumaini TV, aliyeshinda kipengele cha Makala za luninga (TV) 


Pia wapo Averine Kitomari wa Habari Leo, aliyeshinda upande wa Magazeti (Print), Veronica Mrema wa Boresha Radio (Online) aliyeshinda upande wa radio na mshindi wa jumla wa tuzo hizo ni Grace Mwakalinga anayeripotia vyombo vya IPP Media Mkoani Mbeya,.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Andrew Chale, amesema tuzo ni ya maana kubwa kwa Wanahabari za Mtandao (blogs) kwani zimeleta taswira pana ya kuthaminiwa kwa Wanahabari wa mtandaoni.


"Nawashukuru TMDA kwa kuja na tuzo hizi kwa  waandishi kwani zitaleta chachu kwa wengine kwenye kuhabarisha umma kuhusu habari za Udhibiti wa dawa na vifaa tiba." Amesema Chale.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TMDA, Bw. Adam Fimbo amesema


"Taratibu za kutoa tuzo kwa Waandishi wa habari wanaofanya vizuri katika kuandika habari za TMDA, zitaendelea kila mwaka ikiwa ni sehemu ya kufanikisha jukumu la Mamlaka yetu la kuelimisha Umma." amesema Bw. Fimbo.


Awali kabla ya tuzo hizo, kilitanguliwa kwa kikao kazi kwa Wahariri na Waandishi wa Habari, kutoka mikoa ya Njombe, Mbeya, Rukwa na Songwe ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Juma Homera.


Mkuu wa Mkoa Mhe. Homera amewataka Waandishi wa Habari nchini kuzingatia maadili ya Uandishi ikiwemo kufuata misingi mema ya kalamu na sauti zao kwa kutoa habari sahihi na zenye tija kwa jamii ili kujenga taifa imara na lenye afya.


RC Homera amesema, Serikali ipo makini katika kulinda afya za wananchi kupitia TMDA, ambao wamekuwa makini katika kudhibiti bidhaa za dawa, vifaa tiba na vitendanishi pamoja na bidhaa za tumbaku kwa kuhakikisha ubora, ufanisi na matumizi sahihi ya bidhaa hiyo.


"Elimu zaidi inahitajika zaidi kwa jamii, wengi wanatumia dawa pasipo kupewa ushauri wa daktari, Niwapongeze TMDA kwa kuwa na ushirikiano na wanahabari ambao mchango wao katika kupeleka elimu kwa jamii ni kubwa…niwasihi tukatumie vyema kalamu na sauti zetu kwa kutoa taarifa zitakazolinda afya za watanzania.” Amesema.


Kuhusiana na udhibiti wa dawa bandia mkoani humo Homera amesema, wamekuwa wakishirikiana na Mamlaka hiyo mkoani Mbeya katika kupambana na kutokomeza dawa bandia ili kulinda jamii dhidi ya madhara yatokanayo na dawa hizo.


Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba ( TMDA,) Adam Fimbo amesema, katika kikao hicho watatoa elimu, kueleza majukumu yanayofanywa na Wakala hiyo, wajibu wa kila mmoja katika kulinda afya ya jamii kwa kuzuia athari zinazoweza kujitokeza kutokana na matumizi ya Dawa, vifaa tiba na vitendanishi pamoja na kujadiliana kuhusu mahitaji ya wadau ili kuboresha na kutoa huduma bora zaidi.


Pia ameeleza kuwa, elimu kwa Umma kwa Wakala hiyo ni muhimu na wamekuwa wakitoa elimu kwa jamii juu uelewa na matumizi sahihi ya dawa ili kulinda afya na hiyo ni kupitia vyombo vya habari.


Fimbo amesema, licha ya Wakala hiyo kushika nafasi ya kwanza barani Afrika kwa kuwa na mifumo bora ya udhibiti wa bidhaa za dawa, vifaa tiba na vitendanishi bado wanaendelea kusajili, kupima ubora bidhaa kupitia maabara zao ili mlaji apate bidhaa salama bila kudhurika.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI