Matukio katika picha wakati wa Kikao cha 49 cha Baraza kuu la wafanyakazi wa NSSF kilichofanyika jijini Mwanza
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Balozi Ali Idi Siwa, amesema Mfuko utaendelea kusimamia maono ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuhakikisha Watanzania waliopo kwenye sekta binafsi na sekta isiyo rasmi wanasajiliwa na NSSF pamoja na waajiri wanawasilisha michango stahiki ya wafanyakazi wao.
Balozi Siwa alisema hayo jana jijini Mwanza wakati wa ufunguzi wa kikao cha 49 cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa NSSF, ambapo aliwataka watumishi wa Mfuko kuendelea kutoa huduma bora, kujielekeza katika matumizi ya TEHAMA, kushirikiana sehemu za kazi na kuifika sekta isiyo rasmi kwani imebeba sehemu kubwa ya Watanzania ambapo kupitia kundi hilo Mfuko utapata wanachama wengi wapya.
Alisema mpango wa mwaka na bajeti pendekezwa ya Mfuko kwa mwaka wa fedha 2022/23, Mfuko umeweka malengo mbalimbali ikiwemo kusajili wanachama wapya 313,478, kukusanya michango ya shilingi trilioni 1.61 pamoja na kukusanya shilingi bilioni 383.5 ambazo ni mapato yatokanayo na uwekezaji.
Balozi Siwa alisema kwa mwaka wa fedha 2022/23 Mfuko pia umeweka lengo la kulipa mafao mbalimbali kiasi cha shilingi bilioni 828.91 sawa na ongezeko la asilimia 20, na kwamba endapo watafanikiwa kuyaishi maadili ya Mfuko ‘core values’ na kutimiza malengo waliyojiwekea thamani ya NSSF itafikia shilingi trilioni 6.6 ifikapo Juni 30, 2023 ukilinganisha na kadirio la thamani ya shilingi trilioni 5.8 ifikapo Juni 30, 2022.
Aliwataka wajumbe wa baraza hilo wakawe kioo kwa wenzao ili Mfuko uweze kuwa na matokeo chanya kwa wanachama na Mfuko kwa ujumla.
Naye, Ibrahim Maftah ambaye ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, alisema Mfuko umefanya vizuri katika kutekeleza majukumu yake ambayo ni kuandikisha wanachama, ukusanyaji wa michango, kuwekeza na kulipa mafao.
Alisema Mfuko umefanya mapitio ya Mpango wa Uchangiaji wa Hiari ili kuvutia wanachama wapya kutoka katika makundi mbalimbali ya sekta isiyo rasmi ikijumuisha wakulima, wavuvi, wamachinga, mama lishe, waendesha boda boda na bajaji.
"Lengo la mapitio hayo ni kuongeza wigo wa wanachama na kuwa na mafao yanayokidhi mahitaji ya makundi hayo," alisema Maftah.
Maftah alisema katika mwaka huo wa fedha wa 2022/23, Mfuko pia unategemea ongezeko la wastaafu 30,084 kutoka wastaafu 20,894 mwishoni mwa mwaka 2021/2022
Alifafanua kuwa kwa mwaka wa fedha 2022/23, Mfuko umepanga kukusanya kiasi cha shilingi trilioni 1.59 ambazo zitakusanywa kutoka sekta binafsi na shilingi bilioni 15 zitakusanywa kutoka sekta isiyo rasmi.
Kuhusu kulipa mafao, alisema Mfuko pia umejiwekea lengo la kulipa mafao mbalimbali kiasi cha Shilingi bilioni 828.91 sawa na ongezeko la asilimia 20 ukilinganisha na kadirio la kiasi cha Shilingi bilioni 692.46 kwa mwaka wa fedha 2021/22.
Aidha alisisitiza kuhusu uboreshaji wa huduma kwa wateja, matumizi ya TEHAMA katika shughuli za Mfuko, makusanyo ya michango na mapato ya uwekezaji, kujenga utamaduni wa kufanya kazi kwa pamoja (Team work) na usimamizi wa utendaji kazi.
Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Ekwabi Mujungu, alisema watumishi wako tayari kuendelea kutoa huduma kwa mujibu wa taratibu zilizopo.
Kwa upande wake, Willy Kabona ambaye ni Katibu wa TUICO, alisema kazi kubwa ya baraza hilo ni kuishauri Menejimenti kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo kupitia mpango wa Mfuko ya mwaka wa fedha 2022/23 pamoja na makadirio ya mapato na matumizi.
"Tunashukuru kwa somo tosha kutoka kwa mgeni rasmi ambalo litaweza kusaidia kujadili kushauri na hatimae yale yatakayokuwa tumependekeza tutakapokuja kwako kwenye bodi yapate baraka," alisema.
0 Comments