IMEELEZWA kuwa kuwasaidia makundi yenye changamoto au kuwaondolea kero ni moja ya njia ya kuisaidia serikali kuyawezesha makundi hayo.
Akitoa misaada kwa kwa vituo vya Moyo Mmoja na Passion Kamelot Children Home vya Wilayani Bagamoyo wakati maadhimisho ya miaka 58 ya Muungano mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge amesema kuwa jamii inapaswa kuwasaidia watu wenye uhitaji ili nao wajione ni sehemu ya jamii.
Kunenge amesema kuwa jamii ni familia kubwa hivyo kuwasaidia watu wenye uhitaji ni kuisaidia familia.
Amesema kuwa wametoa misaada hiyo ili kuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa akipambana kuhakikisha anapunguza changamoto kwa wananchi.
Aidha amewataka wananchi kushiriki kikamilifu wakati wa zoezi la sensa ya watu na makazi ili nchi iweze kujua idadi ya watu na kupanga bajeti kutokana na idadi ya wananchi wake.
Naye Sister Asteria Pantaleo ambaye ni mlezi wa kituo cha Passion Kamelot Children Home amesema kuwa wananchi wanaokaa jirani na kituo hicho wanamahitaji mengi ya kijamii.
Kwa upande wake Apaisaria Minja Meneja wa kituo cha Moyo Mmoja amesema kuwa wanaomba wanafunzi wanaohitimu elimu ya Msingi wanaotoka kwenye kituo hicho kupangiwa shule za mbali ili kubadili mazingira.
0 Comments