Msemaji wa Sekta ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wa ACT Wazalendo, Pavu Abdallah.
Na Arodia Peter, Matukio Daima APP ,DAR
Chama cha ACT Wazalendo kimeitaka Serikali kuheshimu ustawi wa maslahi ya watumishi wa Umma kwa kuwaongeza mishahara ili waweze kuishi maisha ya raha na furaha.
Hayo yamo kwenye hotuba ya Msemaji wa Sekta ya Utumishi wa Umma na Utawala bora wa chama hicho, Ndugu Pavu Abdallah leo April 22,2022.
Pavu alikuwa akichambua bajeti ya Wizara Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa mwaka 2022/2023.
Akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya chama hicho leo jijini Dar es Salaam, Pavu amesema kuwa
mishahara ya Watumishi wa Umma nchini haijapandishwa tangu 2014 licha
ya kupanda kwa gharama za maisha kila mara.
Amesema kutokana na Serikali kutokupandisha mishahara ya Watumishi wa Umma kwa miaka saba mfululizo watumishi wa umma wameendelea kuishi kwa mishahara midogo isiyoendana na uhalisia wa kumudu mahitaji yao.
"Ongezeko la mishahara ya wafanyakazi ni takwa la kisheria, si la Utashi wala hisani ya kiongozi mmoja katika nchi, kauli za huko nyuma za serikali zinaonyesha hadaa juu ya jambo hili" amesema na kuongeza kuwa:
....awali, serikali iliahidi kuongeza mishahara baada ya kukamilisha uhakiki wa wafanyakazi ambao ungefanyika ndani ya miezi miwili, kisha pia Serikali ingeendelea kulipa malimbikizo ya madeni ya wafanyakazi na kuajiri wengine wapya lakini haikufanya hivyo" amesema Pavu.
Aidha Msemaji huyo wa kisekta ameainisha
Ilani ya ACT Wazalendo ya 2020 ambayo ilikusudia kuthamini Watumishi wa Umma na mchango walionao katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Ilani hiyo iliweka wazi kwamba ACT Wazalendo inaamini, Serikali inatakiwa kuheshimu ustawi na maslahi ya Watumishi wa Umma ili waweze kuishi maisha ya raha na furaha. Hili linawezekana tuu endapo Watumishi wa Umma watalipwa mishahara inayowawezesha kumudu gharama za maisha.
Kwa muktadha huo Pavu amesema ACT Wazalendo inaitaka Serikali kupambanua mikakati na sera zake kwa kujali maslahi ya Watumishi wa Umma huku akitoa wito kwa shirikisho la vyama vya wafanyakazi nchini (TUCTA) kuongoza madai yao ya kisheria kila uchao
bila kusubiri risala za Mei Mosi za kila mwaka.
"Hotuba ya Waziri wa Utumishi na Utawala bora bado haijasema wazi ni namna gani Serikali itashughulikia stahiki za watumishi wa umma.
Malimbikizo ya mishahara, madeni na stahiki zilizotakiwa kulipwa kwa Watumishi wa Umma zimefikia shilingi bilioni 429.80 mwaka 2020/2021 kutoka shilingi bilioni 334.15 mwaka wa fedha 2019/2020. Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 28.
"Aidha taarifa ya CAG imegundua jumla ya Sh. Billion 492 ni malimbikizo ya mishahara na stahiki nyingine walizotakiwa kulipwa baadhi ya watumishi wa umma. Kwa mujibu wa kanuni Na. 23 ya Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma ya mwaka 2009, madai ya Watumishi yanatakiwa yalipwe mara tu yanapotokea.
"Hata hivyo, CAG ameonyesha kuwa madai yanayotokana na watumishi kutolipwa kwa wakati, malimbikizo ya mishahara ya waajiriwa wapya, waliopandishwa madaraja, makato na posho za watumishi yamefikia shilingi bilioni 429.
Hii inadhihirisha sababu za kuporomoka kwa ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi na taasisi za Serikali kwa sababu ari ya watumisi wa umma imeshuka,
ACT Wazalendo tunaitaka Serikali iwalipe Watumishi wote malimbikizo ya madai yao mara moja ili kuwawezesha kukabiliana na gharama za maisha ambazo zimeendelea kupanda."amesema Pavu.
Mbali na hoja hizo, ACT Wazalendo inapendekeza
malimbikizo ya madai ya Wafanyakazi wa Umma yatambuliwe katika takwimu za deni la taifa na Serikali itazame uwezekano wa kuweka sokoni Bondi maalumu kwa ajili ya kupata Fedha za kulipa malimbikizo yote kwa mkupuo na kuweka mfumo ambao utahakikisha kuwa hakuna madeni mapya yanayozalishwa siku za usoni.
0 Comments