Na Amon MtegaSongea .
AFISA Mfawidhi wa kituo cha ufugaji viumbe maji wakiwemo Samaki katika mabwawa ya Ruhila yaliyopo Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma Emmanuel Maneno amewataka wakazi wa Mkoa huo kutumia fursa ya kwenda kujifunza namna ya ufugaji wa Samaki pamoja na kujipatia mbegu za samaki hao ili waweze kuwa wafugaji bora.
Wito huo ameutoa wakati akitoa Elimu juu ya tabia za viumbe maji hasa Samaki kwa baadhi ya wakufunzi wa kutoka vyuo vya taasisi za uvuvi (FETA) ambao wamepata mafunzo ya siku nne yaliyofanyika Manispaa ya Songea Mkoani humo.
Maneno wakati akitoa elimu hiyo amesema kuwa kupitia kituo cha viumbe maji cha Ruhila ambacho ni cha kanda ya kusini ni sehemu ya fursa tosha kwa wakazi wa Mkoa wa Ruvuma kwenda kujifunza namna ya kufugaji bora samaki ambao utawaongezea uchumi kwenye jamii.
Amefafanua kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongonzwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha kituo hicho na sasa kunajengwa jengo la kisasa la kutotolesha mayai ya samaki ambapo hadi sasa imeshafikia zaidi ya asilimia 70 za malengo.
Naye Afisa Uvuvi wa kituo cha Ruhila Lucka Mgwena amewataja aina ya vifaranga vya samaki vinavyozalishwa kwenye kituo hicho kuwa ni Sato na Kambale huku kifaranga kimoja kinauzwa kwa bei ya sh.100 hadi sh.150 na kuwa eneo hilo hadi sasa lina mabwawa 14 .
Mgwena amesema kuwa kituo hicho kinahudumia vifaranga vya samaki katika mikoa ya nyanda za juu kusini ambayo ni Njombe,Iringa,Mbeya ,Rukwa ,Katavi na Ruvuma yenyewe na kuwa vifaranga hivyo havipatikani sehemu nyingine zaidi ya kwenye kituo cha Ruhila kilichopo mkoa wa Ruvuma.
Kwa upande wake Wakala wa elimu na mafunzo ya uvuvi (FETA) Peter Masumbuko amesema kuwa wametoka vyuo mbalimbali kikiwepo na cha Nchi ya Kenya kwa lengo kujifunza zaidi tabia za viumbe maji hasa Samaki ili kuongeza uelewa zaidi pindi wanapofundisha kwenye vyuo vyao wanakofanyia kazi.
Mmoja wa wakufunzi Severia Spring kutoka Uswisi ambaye anafanya kazi Nchi ya Kenya amesema kuwa wamepata fursa kubwa ya kujionea na kuwa ufugaji wa Samaki utawafanya wakazi wa mkoa wa Ruvuma kupata kiteweo hicho ambacho chenye protini nyingi Mwilini.
Naye Proscovia Alando ambaye naye ni kutoka Kenya amefurahishwa na mazingira ya Tanzania kuwa yanavutia kwa ufugaji wa Samaki na kuwa anashangazwa kuona baadhi ya watanzania kuto kuitumia fursa hiyo kwa umakini wakati maeneo yapo ya kutosha.









0 Comments