Baadhi ya madiwani kutoka katika kata 12 za halmashauri ya Moshi zinazohudumiwa na mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira mjini Moshi(MUWSA) wamekiri kupunguziwa majukumu yaliyokuwa yakiwaelemea kuhusiana na huduma ya maji.Mwandishi Gift Mongi,MDTV Arusha
Katika kuboresha huduma zake mamlaka hiyo imekasimisha baadhi ya majukumu yake kwa ofisi za watendaji kata ambapo wananchi wataweza kusikilizwa na kupata utatuzi wa baadhi ya changamoto badala ya kufunga safari hadi zilipo ofisi za MUWSA.
Daniel Pius diwani wa kata ya Mwika Kisini alisema mamlaka hiyo imewarahisishia baadhi ya madiwani kwani walikuwa wakiulizwa maswali juu ya upatikanaji wa huduma za MUWSA na kwa kuwa walikuwa hawana uelewa iliwawia vigumu kutoa majibi sahihi.
"Sisi ni wawakilishi wa wananchi Sasa wanapotuuliza juu ya upatikanaji wa huduma ya maji au kero nyingine hatukuwa na majibu yakieleweka lakini Sasa kazi ni rahisi watapata majibu kwa mtendaji kata"alisema
Samweli Shao diwani wa Mwika Kaskazini alisema utaratibu ulioanzishwa na MUWSA kutoa taarifa katika ngazi ya kata ni mzuri na kuwa utaepusha usumbufu waliokuwa wakiupata madiwani pamoja na wananchi kusafiri hadi zilipo ofisi za mamlaka ambapo gharama zilikuwa zikitumika.
Anna Lyimo ambaye ni diwani wa Kilema Kaskazini alisema kwa kipindi kirefu wananchi wa kata yake walikuwa wakikosa taarifa sahihi juu ya huduma zitolewazo na MUWSA jambo lililopelekea wengine kupata taarifa ambazo sii sahihi lakini kwa sasa mambo yataenda kubadilika na kuwa hata huduma ya maji itaenda kupanuliwa wigo wake.
Kaimu mkurugenzi wa MUWSA Edes Mushi alisema mamlaka hiyo kupitia mkataba wa huduma kwa mteja unaeleza wazi kabisa kuwa mteja atakuwa na haki zipi pindi akiwa mteja na kama zikikiukwa afanyeje
"Katika kuiunganksha mamlaka na jamii tunayoihudumia ndio maana kuna huu mkataba wa huduma kwa mteja ambao ni kiunganishi kati yetu sisi kama mamlaka lakini na watu tunaowahudumia na hapa mambo yote yapo ikiwemo haki za pande zote mbili na hata wajibu pia"alisema
Kwa mujibu wa Mushi ni kuwa mkataba huo umekuwa ukimalizika kila baada ya miaka mitatu na pindi unapotengenezwa mwingine mbali na kuwa shirikishi lakini pia huboreshwa kulingana na mahitaji ambayo jamii inataka.
Afisa uhusiano wa MUWSA Flora Nguma alisema kuwa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira mjini Moshi ni taasisi ya kiserikali yenye jukumu la kusambaza majisafi na uondoaji majitaka katika manspaa ya Moshi.
Alisema mkataba wa huduma kwa mteja ni takwa la kisheria na kuwa katika uandaaji wake linatakiwa kuwa shirikishi baina ya pande zote mbili yaani kwa upande wa mamlaka(mtoa huduma) na mteja(mtumia huduma)na kuwa unaeleza wajibu wa pande zote mbili
"Tumeona ni vyema tukaanza na hawa watendaji wa kata kuwapitisha katika mkataba huu kwani ndio wasimamizi wakuu wa huduma ikiwemo maji katika ngazi za chini kabisa na itakuwa rahisi kwa wananchi kuweza kupata majibu ya maswali yao kule chini katika mitaa yao" alisema
0 Comments