KAMATI ya Amani ya mkoa wa Pwani imemuombea Rais Samia Suluhu Hassan Mungu kumuepusha na changamoto wakati wa utekelezaji majukumu ya kuiletea nchi maendeleo na wamemwombea Rais Hayati John Magufuli ili Mungu amrehemu.
Aidha wametoa tamko la kulaani vitendo vya ukatili wa kijinsia na mauaji hapa nchini na kuiomba serikali kuwashirikisha kwenye usuluhishi wa migogoro inayojitokeza ndani ya jamii.
Akizungumza Mjini Kibaha wakati wa ibaada na dua kwa ajili ya viongozi, serikali nchi na dunia kwa jumla Mwenyekiti mwenza wa Kamati hiyo Padri Beno Kikudo alisema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amefanya mambo makubwa ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.
Kikudo alisema kuwa licha ya nchi kupita kwenye changamoto nyingi ikiwemo kumpoteza Rais aliyekuwa madarakani, ugonjwa wa Covid-19 na majanga mbalimbali lakini Rais alisimama imara bila ya kutetereka kuhakikisha nchi inaendelea kusonga mbele.
Alisema kuwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeweza kufanya mambo mengi ya kimaendeleo ikiwemo ujenzi wa madarasa yatokananayo fedha za mapambano ya ugonjwa wa Covid-19.
"Sisi kama viongozi wa dini tumeona kazi kubwa iliyofanywa na Rais wetu tumeona tumuunge mkono kwa kumfanyia maombi kwa madhehebu yetu yote pia tunaiombea serikali nchi na dunia ambayo kwa sasa kuna vita kule Ukraine na Urusi,"alisema Kikudo.
Aidha alisema kuwa Hayati Rais John Magufuli alikuwa ni kiongozi mahiri ambapo katika kipindi cha utawala wake aliweza kufanya miradi mikubwa ikiwemo ile ya sekta ya ujenzi ikiwemo treni ya mwendokasi SGR, barabara za juu, mradi wa uzalishaji umeme Bwawa la Mwalimu Nyerere, barabara mbalimbali na miradi mingine.
Kwa upande wake mwenyekiti mwenza wa kamati hiyo Sheikh Hamis Mtupa alisema kuwa serikali iwashirikishe kwenye kutatua baadhi ya migogoro kwani wanaokinzana ni waumini aidha wa makanisa au misikiti.
Mtupa alisema kuwa moja ya mgogoro ambao waliutatua ni wa wafanyabiashara wa eneo la Picha ya Ndege ambao walitaka kufanya maandamano kwa madai sehemu wanayopelekwa halina biashara lakini eneo la mwanzo walilokuwa wakifanyia biashara ni hifadhi ya barabara.
Awali mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge alisema kuwa kamati hiyo ni muhimu sana kwani mbali ya kuwafundisha waumini kuachana na uovu pia inafanya maombi kumwomba Mungu kuwafanya wanadamu kuwa hofu yake.
Kunenge alisema kuwa duwa na sala zinazofanywa na viongozi wa dini zinasababisha uwepo wa amani na utulivu ndani ya nchi kwani bila ya viongozi hao maadili yangekuwa ni mabaya.
0 Comments