Na Gift Mongi
Kukosekana kwa usimamizi madhubuti wa kisera na kimfumo kunatajwa kuwa ni miongoni mwa sababu zinazopelekea sekta ya ngozi nchini kuendelea kuzorota siku hadi siku jambo linalotishia uhai wa biashara hiyo.
Wadau wa sekta hiyo wanasema kama sio kushamiri kwa vikwazo hivyo kungeweza kusaidia kuanzishwa kwa viwanda vingi vidogovidogo ambavyo mbali na kuzalisha ajira pia kungechangia kuimarika kwa soko la ndani la bidhaa za ngozi.
Takwimu zinaeleza kuwa Tanzania ni nchi ya tatu kwa barani Afrika kwa kuwa na idadi kubwa ya mifugo ikitanguliwa na Afrika Kusini pomoja na Ethiopia ambao wote wapo katika orodha nzuri ya kuwa na idadi ya mifugo.
Kwa mantiki hiyo ni dhahiri uwepo wa idadi kubwa ya mifugo kunaweza kuongeza malighafi yatokanayo na mazao ya mifugo kama nyama,kwato,na hata ngozi ambazo hutumika katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo yaani uzalishaji au utengenezaji bidhaa.
Rajab Mfinanga mkazi wa Kileo wilayani Mwanga ambaye ni muuzaji wa ngozi anasema biashara hiyo kwa sasa inaenda kwa kusuasua na jambo ambalo lisipowekewa umakini wa ziada itaenda kufa.
Anasema kutokana na kukosekana kwa soko lenye uhakika la ndani kwa kiasi kikubwa imechangia wafanyabiashara wasio waaminifu kutumia njia za panya na kutorosha ngozi nje ya nchi.
"Hakuna soko la uhakika tozo zimekuwa nyingi sasa wafanyabiashara badala ya kukusanya ngozi na kuiuza katika soko la ndani baadhi wasio waaminifu wamekuwa wakitumia njia za panya na kuiuza nje ya nchi na kisababisha uhaba wa bidhaa hiyo" alisema
Anasema kutokana na hali ilivyo huenda viwanda vya ndani vinavyozalisha bidhaa za ngozi vikakosa malighafi kwani ngozi nzuri yote ndio inayopelekwa nje ya nchi kimagendo na inayobaki ni kama makapi haifai katika uzalishaji.
Mkurugenzi wa kiwanda cha Woisso Original Products (WOP)Keneth Woisso anasema kwa siku za karibuni biashara ya ngozi inapita katika wakati mgumu kwani ngozi zimeadimika na nyingi zinasafirishwa nje ya nchi.
Anasema ngozi nzuri yote imekuwa ikisafirishwa nje ya nchi na inayosalia ni mbovu haifai kwa matumizi ya uzalishaji na kuiomba serikali kuona namna ya kukabiliana na tatizo hilo lengo likiwa ni kuvinusuru viwanda vya ndani ambavyo pia vinazalisha ajira.
"Sisi wazalishaji wa bidhaa za ngozi kwa siku za karibuni tunapitia kipindi kigumu kwani hakuna malighafi na hata ukipata zipo chini ya kiwango yaani hazifai katika uzalishaji wa bidhaa" alisema Mkurugenzi hiyo wa WOP.
Anasema katika Sekta hiyo ya ngozi kwa sasa zipo changamoto kuu mbili ambayo ni asilimia 10 ya kodi ya huduma (export levy)kwenye ngozi iliyosindikwa hadi kufikia wett blue
Wakati changamoto nyingine ni asilimia 80 kodi ya huduma (export levy)kwenye ngozi ghafi ambapo kiwango hiki kikipungua huenda biashara hiyo ikawa katika sehemu sahihi zaidi ya hapa ilipo.
"Kutokana na kiwango hiki kikubwa cha kodi kumepelekea ngozi nyingi kubaki mikononi mwa wafanyabiashara huku sisi tunaohitaji kama malighafi tukizikosa" anasema Woisso
Woisso anasema kutokana na hali hiyo kwa sasa ipo haja kwa serikali kuangalia changamoto hizi kwa undani na kutoa suluhisho ili kuweza kudhibiti baadhi ya waganyabishara kuingiza au kuiuza ngozi kwa njia ya magendo.
Kuhusiana na hali ya soko la bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya ndani anasema tayari wananchi wamehamasika sana kununua bidhaa zinazozalishwa nchini tofauti na kipindi cha nyuma ambapo bidhaa za nje zilitesa sokoni.
Alisema kwa hivi sasa ubunifu umekuwa ni mkubwa jambo ambalo limefanya kuaminiwa na kuzalisha bidhaa mbalimbali vikiwemo viatu vya majeshi mbalimbali na hata viatu vya kawaida na bidhaa nyinginezo
''Tunatengeneza viatu vya majeshi na hawaagizi tena nje ya nchi hii ni fursa mpya katika kukuza soko la ndani na kukuza sekta ya ngozi nchini kwa ujumla wake na hali inaelekea kuwa nzuri ''alisema Woisso.
Anasema kiwanda cha WOP katika kuunga mkono jitihada za serikali kuelekea uchumi wa viwanda wamejidhatiti kutengeneza bidhaa zenye ubora wa kimataifa ili kukuza soko la bidhaa za ngozi ndani na nje ya nchini.
0 Comments