Maafisa wa Ukraine wanasema wamemuua jenerali wa nne wa Urusi katika ishara kwamba makamanda wa Moscow wanazidi kulazimishwa kuongoza vita kutoka mbele.
Anton Gerashchenko, mshauri katika wizara ya mambo ya ndani ya Kyiv, alidai kwenye Telegram kwamba vikosi vya Ukraine vilimuua Meja Jenerali wa Urusi Oleg Mityaev wakati wa mapigano makali viungani mwa mji wa kusini-mashariki wa Mariupol.
BBC haiwezi kuthibitisha dai hili kwa uhuru na Moscow bado haijatoa maoni yoyote kuhusu ripoti za kifo chake.
Gerashchenko aliandika kwamba Mityaev alikuwa kamanda wa kitengo cha 150 cha bunduki na akachapisha picha ya kile alichosema kuwa afisa aliyekufa.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky pia aliripoti kifo cha jenerali mwingine wa Urusi wakati wa hotuba yake ya usiku kutoka Kyiv, lakini hakumtaja jina.
Urusi inaaminika kuwa na Majenerali Meja wapatao 20 nchini Ukraine wanaoongoza vita .
Wakati huo huo Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskly amewataka moja kwa moja maafisa wakuu wa Urusi na wanahabari kujiuzulu nyadhifa zao na kuchukua msimamo dhidi ya uvamizi wa nchi yake.
Akizungumza wakati wa hotuba ya usiku kutoka mji mkuu wa Ukraine wa Kyiv, Zelensky alihutubia moja kwa moja "maafisa wote wa Shirikisho la Urusi"."Ikiwa utasalia ofisini, ikiwa haupingi vita, jumuiya ya kimataifa itakunyima kila kitu," Zelensky alisema. "Kila kitu ambacho umepata kwa miaka mingi. Hili tayari linafanyika."
0 Comments