Rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump ameibuka kwa mara ya kwanza na kuzungumzia vita inayoendelea baina ya Urusi na Ukraine ambapo amepinga vikali hatua ya Rais Vladimir Putin kuivamia Ukraine.
Trump amesema alimchukulia kawaida Putin alipoanza kupeleka vikosi vya majeshi mpakani mwa Ukraine akiamini ilikuwa ni kwa lengo la kutengeneza mazingira ya majadiliano baina yake na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy.
Katika mahojiano aliyoyafanya na Gazeti la Washington Examiner la Marekani kwa njia ya simu, Trump amesema ameshangazwa na hatua ya Putin ya kuivamia Ukraine. “ImenishangazaNilifikiri ilikuwa ni mbinu ya majadiliano baada ya Putin kupeleka vikosi kwenye mipaka ya nchi yake na Ukraine na nadhani ilikuwa ni njia ngumu lakini ilikuwa ni nzuri kwa kufanyia majadiliano,” amenukuliwa Trump.
Trump ambaye alikuwa na uhusiano wa karibu na Putin wakati wa utawala wake, amedai kwamba Putin amebadilika sana tangu wawili hao walipofanya kazi pamoja.
Rais huyo wa zamani wa Marekani, amekuwa akikosolewa vikali kutokana na namna anavyomchukulia Putin hasa anavyoshindwa kutamka na kukemea hadharani kitendo cha Putin kuivamia Ukraine.
0 Comments