Teddy Kilanga _Arusha
Kufuatia athari za janga la ukame la muda mrefu ulioathiri baadhi ya maeneo ya Tanzania,Mkuu wa wilaya ya Longido,Nurdin Babu amewataka wananchi kutobweteka katika kipindi hiki cha mvua ili kuondokana na janga la njaa liliowakumba miezi sita iliyopita.
Akizungumza februari 25,2022 katika hafla ya kukabidhi chakula kilichotolewa na shirika World vision kupitia mradi wa Kitumbeine (AP)Babu amesema kutokana na wilaya hiyo kukabiliwa na hali ya ukame na kusababisha vifo vya mifugo ambapo zaidi ya ng'ombe 200 pamoja na kondoo na mbuzi 356 walikufa kutokana na ukosefu wa chakula na maji.
Aidha amesema kuwa kutokana na hali hiyo wananchi wamepungukiwa na chakula na uzalishaji umepungua wilayani humo kutokana na mabadiliko hayo ya hali ya hewa hivyo wanashukuru shirika hilo kwa kutoa msaada wa chakula zipatazo tani 20 za unga wa mahindi pamoja na maharage tani 5.
Babu amesema kutokana na janga hilo wamejipanga kuhakikisha katika kipindi cha mvua wanahamasisha wananchi katika shughuli za kilimo na kuwaelimisha namna ya kuweka akiba ya chakula ikiwa serikali kupitia idara ya kilimo imetenga bajeti ya mbegu ili kuwasaidia kulima mazao yaliyo bora.
"Niwaombe wananchi wa wilaya ya Longido kutokubweteka kwani misaada hiyo ya chakula haitakuwepo siku zote wachukue fursa ya msimu huu wa mvua kuendelea kupanda mazao ambayo yatawasaidia baadaye,"alisema Babu.
Awali akitoa taarifa katika hafla hiyo Mratibu wa mradi wa worldvision wa Ketumbeine(AP)Peruth Daud amesema zaidi ya kaya 900 katika tarafa ya Ketumbeine iliyoko wilayani Longido mkoani Arusha zimepatiwa chakula na shirika la world vision ili kupunguza janga la njaa.
Daud amesema chakula hicho ni maharage na unga wa mahindi ambapo wamepatiwa kupitia kata zilizopo katika tarafa hiyo ikiwemo Ketumbeine,Elangatadapash,Noondoto,Gilailumbwa,Gilabomba na Ilerienito.
Alisema jumla ya tani 20 za mahindi na tani 5 za maharage vyenye thamani ya sh.milioni 41.4 na kunufaisha kaya 1000 ndani ya vijiji 19 katika Tarafa hiyo.
"Kila kaya nufaika itapata kilogramu 20 za unga wa mahindi na kilogramu tano za maharage ambapo watoto 3214 pia watanufaika,"amesema Mratibu huyo.
Amesema mbali na msaada huo watashirikiana na wataalamu wa ngazi ya wilaya,kata pamoja na viongozi wa vijiji wataendelea kutoa mafunzo kwa wananchi wa tarafa hiyo juu ya kukabiliana na majanga mbalimbali likiwemo la ukame.
Naye mmoja wa wananchi wa Tarafa ya Kitumbeine ambaye pia ni kiongozi wa mila,Peter Mollel amesema mabadiliko ya hali ya hewa imewaathiri kwa kiasi kikubwa hali iliyopelekea wanaume kukimbia familia zao kutokana janga la njaa lililosababishwa na ukame.
"Tunawashukuru serikali na wadau wa shirika la World vision kutupatia chakula pamoja na mifugo ambayo imeanza kutusaidia kwani hali ya wilaya hii ilikuwa mbaya sana,"amesema.
0 Comments