Header Ads Widget

UTANI NA KUMBUKUMBU MAHAKAMANI

 


Adeladius Makwega-DODOMA


Katika sheria ya makosa ya Jinai ya Tanganyika, utani ulikuwa si kosa la jinai, kwa hiyo kwa sehemu kubwa ilikuwa vigumu mno kuweza kupata nakala za mashauri ya utani katika Mahakama za Wilaya na Mahakama ya Hakimu Mkazi, huku ukibahatisha kumbukumbu hizo katika Mahakama za Mwanzo.


Kwa kuwa utani ulikuwa katika sheria za kimila tu, pahala pekee ambapo utani uliweza kuonekana nakala zake ni Mahakama za Mwanzo kwa bahati nasibu kama nilivyokwambia. Mwaka 1962 machifu walipokonywa mamlaka yao ya utawala na uhakimu, ndipo na utani huo ukawa sehemu ya Sheria ya Makosa ya Jinai ya Tanzania.


Tangu mwaka 1963 hadi 1973 yaani miaka kumi baadaye, mashauri mengi ya utani yaliaanza kuongezeka katika meza za mahakama zetu kama anavyosema Stephen A. Lucas-Utani Relationships in Tanzania Volume Seven, 1976- Dar es Salaam.


Hilo linaungwa mkono na Ndugu E .R Mchatta- A note on Utani in the Legal Field, 1971 Dar es Salaam wakati akifanya utafiti wake juu ya utani katika mashauri yaliyowahi kupelekwa mahakamani.


Ndugu huyu anasema kuwa watumishi waliowahi kutumikia mahakama walimuuma sikio na kumwambia kuwa kulikuwa na utaratibu mbaya wa namna ya kuhifadhi kumbukumbu za mahakama.


“Nilishauriwa njia nzuri ya kutambua mashauri mbalimbali yaliyowahi kupelekwa mahakamani ni kuwatafuta wale waliowahi kuwa watumishi wa Mahakama za Mwanzo na waliowahi kushirikiana nao kama vile mahakimu, wazee wa baraza, maafisa wa polisi wanaweza kulisimulia hilo vizuri.”


Kwa hiyo ndugu Mchatta alisema kuwa aliwajibika kuwa na orodha ya mahakama kadhaa za mwanzo na majina ya waliowahi kutumikia chombo hiki. Akiwa katika utafiti wake, kigulu na njia, alimpata Liwali wa zamani wa Dar es Salaam. 


Liwali huyu alikumbuka mashauri kadha ya utani ya tangu mwaka 1961 kwa mdomo bila ushahidi.


Alisimuliwa kuwa katika shauri moja kuna jamaa aliyevali nguo zake nje ndani alipokonywa nguo hizo na watani wake. Kulingana na sheria za kimila hapa hakukuwa na wizi bali huo ulikuwa utani tu. Kubwa mbele ya mahakama, ilikuwa ni kuhakisha kuwa watu hao wawili ni watani tu. Kwa hiyo aliyepokonywa nguo alishindwa shauri hilo.


Huku Liwali huyo wa zamani wa Dar es Salaam alimsimulia shauri lingine ambapo yalitolewa matusi ambayo yule aliyetukanwa alishindwa shauri hili, kwani aliyetukana alikuwa mtani hii ni kabla ya mwaka 1962


Ndugu Mchata katika utafiti wake alisimuliwa kuwa kuna shauri lingine, polisi mmoja ambaye alikuwa akifanya kazi hiyo huko Njombe mwaka 1966.


“Siku moja meneja mmoja wa chama cha ushirika Njombe aliwasha gari lake hadi kituo cha mafuta, alipofika hapo aliagiza kuwekewa mafuta katika gari lake. Kwa hakika muhudumu wa kituo hicho alifanya kazi hiyo kama kawaida yake. Mara baada ya kuwekewa mafuta, meneja aliondoa gari lake na kumfurumushia matusi ya nguoni dada huyo.”


Matusi hayo yalimkwaza mno muhudumu wa kituo cha mafuta na alilipeleka shauri hili polisi ili kufanyiwa kazi. Kama kawaida, shauri lilipokelewa na kusajiriwa katika kitabu cha polisi.


Polisi aliyepokea shauri hilo alifanya uchunguzi wa awali, alimpigia simu meneja huyu wa chama cha ushirika Njombe. Waswahili wanasema hasidi haachi asili yake.


“Meneja alipoisikia sauti ya polisi huyu ikiwa matamshi ya Kingoni, aliutua mzigo mwingine wa matusi kwa afisa huyu wa polisi.”


Shauri hilo lilipelekwa mbele mahakamani, hakimu alikutana uso kwa uso na mtuhumiwa aliyeshitakiwa kwa kuwatusi muhudumu wa kituo cha mafuta na afisa wa polisi huku akitekeleza majukumu yake.


Mbele ya mahakama shauri lilisikilizwa na kila upande kupewa nafasi ya kueleza, meneja huyu wa chama cha ushirika alijitetea kuwa hao wote aliodaiwa kuwatusi walikuwa ni Wangoni na yeye alikuwa Mnyamwezi, kwa kuwa kuna utani mkubwa baina ya WANGONI na WANYAMWEZI alidai hakuwa na kosa lolote lile mbele ya mahakama tukufu.


Mahakama ilimtia hatiani meneja huyu wa chama cha ushirika Njombe, kwakulipa shilingi 50 na kujitetea kwake kwa utani wa makabila haya mawili hakukumsaidia lolote.


Hayo ni mambo ya mashauri hayo. Je leo nina hoja gani?


Mwanakwetu swali la leo ubaoni ni, Je mafaili na kumbukumbu zote za mahakama zetu za mwanzo yanahifadhiwa vizuri?


Macho hayana pazia, tukipita katika mahakama zetu nyingi za mwanzo, mandhari ni ile na kurundikana na mafaili ya zamani. Pengine kulitafuta faili la shauri la mwaka 1987 ni vigumu kulipata, hata kama utatoa bakishishi ya dhahabu, mwanakwetu hata kama utatoa bakishishi ya dhahabu.


Natambua kuwa mahakama za zote za juu kumbukumbu hizo zinahifadhiwa vizuri. Ifahamike wazi kuwa mashauri mengi yanafanyika katika ngazi ya chini ambayo ni Mahakama ya Mwanzo na huko ndipo ilipo jamii ya Watanzania walio wengi.


Nashauri watendaji wa ngazi hii wapatiwe vifaa vya kisasa na mafaili yote ya zamani yaingizwe katika kumbukumbu zisizoharibika na zinazotafutika kwa haraka kama za Mahakama Kuu, narudia kama za Mahakama Kuu.


Kwa kufanya hivyo habari ya kuwatafuta waliowahi kufanya kazi na mahakama kupata taarifa za mahakama za mwanzo itabaki katika kaburi la sahau.


Nakutakia siku njema.


makwadeladius@gmail.com

0717649257

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI