Header Ads Widget

KPC YAWAKUMBUSHA WANANCHI KUTOA TAARIFA JUU YA VITENDO VYA UKATILII







 


KUFUATIA matukio ya vitendo vya ukatili na mauaji kuendelea nchini Kituo Cha Msaada wa Kisheria Kibaha (KPC) kimewakumbusha wananchi kutoa taarifa za vitendo vya ukatili ili kupunguza matukio ya mauaji.


Hayo yalisemwa mjini Kibaha na mhasibu wa kituo Humphrey Munuo kwa niaba ya Mkurugenzi wa kituo hicho wakati wa utoaji wa elimu juu ya kukabili vitendo hivyo kwa wananchi wa kata ya Mkuza.


Munuo alisema kuwa moja ya changamoto ambazo zinasababisha kuendelea kwa matukio hayo ni jamii kukaa kimya pale vitendo hivyo vinapokuwa haviripotiwi.


"Ili kupunguza matukio ya vitendo vya ukatili ndani ya jamii ni kuyasema kwa kutoa taarifa kwenye vyombo vinavyohusika lakini kukaa kimya ni kusababisha ukatili kuendelea na kusababisha mauaji,"alisema Munuo.


Alisema kuwa vitendo hivyo vya ukatili ikiwa no pamoja na vipigo, ubakaji, ulawiti, kuchoma moto na vile vinavyoambatana na hivyo husababisha jamii kuona kuwa ni vitu vya kawaida jambo ambalo husababisha mauaji.


"Jamii kwa pamoja inapaswa kukemea vitendo hivyo na vinginevyo kwa kutoa taarifa kwa uongozi wa Kijiji, mtaa, wasaidizi wa sheria au vyombo vya dola pale wanapoona mwanajamii anavifanya na si kukaa kimya,"alisema Munuo.


Aidha alisema kuwa matukio ya ukatili ni mengi lakini jamii imekuwa ikikaa kimya na kufumbia macho kwani ukatili huanza kidogo kidogo na kama hatua hazijachukuliwa husababisha mauaji.


Kwa upande wake Mwalimu wa Shule ya Sekondari Nyumbu Fredrick Chagoha alisema kuwa njia nyingine ya kukabili vitendo hivyo ni watu kuwa na hofu ya Mungu na kuweka hisia za mambo mazuri kwenye mioyo yao.


Chagoha ambaye pia ni mtaalamu wa Saikolojia alisema kuwa mtu anapowaza mambo mabaya ndiyo yanayosababisha kufanya vitendo vibaya ikiwemo ukatili na mauaji ambayo hutokana na mvuto wa mawazo mabaya ambapo ni zao la uchungu.


Alisema kuwe na mtazamo wa kuacha namna ya maongezi na kuacha kuongelea mauaji jamii utaona ni jambo la kawaida na kuongelea masuala ya maendeleo na kusaidiana kujengana na kupeana matumaini na si kuharibiana.


Naye mkazi wa Mkuza Martha Mola alisema kuwa wao kama wanajamii wamepata uelewa kwani walikuwa hawajui baadhi ya vitendo kuwa ni ukatili.


Mola alisema kuwa baadhi ya wanajamii wamekuwa ni waoga kutoa taarifa ya vitendo hivyo wakiwemo wanawake huku wakiona kuwa kikubwa ni kuwa wavumilivu na kusababisha vitendo hivyo na kuahidi kuwa mabalozi wa kufichua mambo hayo.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI