Header Ads Widget

KAMATI ZA ULINZI WA WANAWAKE NA WATOTO NGAZI YA MKOA ZATAKIWA KUANDAA MIKAKATI ITAKAYOSAIDIA KUIMARISHA UTENDAJI WA KAZI

 




Na Hamida Ramadhan Dodoma


WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum,Dkt. Doroth Gwajima amezielekeza kamati za ulinzi wa wanawake na watoto ngazi ya Mkoa kuandaa mikakati madhubuti iliyoboreshwa itakayosaidia kuimarisha utendaji kazi ikiwemo kukamilisha uundwaji wa Kamati hizo na kuzijengea uwezo ili zitekeleze majukumu yao ipasavyo kwa lengo la kutokomeza vitendo vya ukatili.


Maagizo hayo ameyatoa leo Februari 15,2022,Jijini hapa wakati akizungumza katika kikao  kazi na viongozi wa Mpango  wa Kitaifa  wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na Watoto (MTAKUWWA) Mkoa wa Dodoma.


Waziri Gwajima amezielekeza kamati za ulinzi wa wanawake na watoto ngazi ya Mkoa  kuandaa mikakati madhubuti iliyoboreshwa  na itakayosaidia kuimarisha utendaji kazi  ikiwemo kukamilisha uundwaji wa Kamati hizo na kuzijengea uwezo ili zitekeleze majukumu yao ipasavyo kwa lengo la kutokomeza vitendo vya ukatili.


Pia,amezielekeza kuhakikisha rasilimali fedha zinatengwa na kutolewa kwa ajili ya utekelezaji wa afua za MTAKUWWA kama inavyoelekezwa katika Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali unaotolewa kila mwaka na Wizara ya Fedha na Mipango.


“Kubainisha wadau wanaotekeleza afua mbalimbali katika Mkoa zinazolenga kupambana na vitendo vya ukatili na uimarishaji wa uchumi wa kaya ili kushirikiana nao katika jitihada za kutokomeza vitendo vya ukatili kwenye jamii ikiwemo kudhibiti wimbi la watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani,”amesema.


Katika hatua nyingine,Waziri Gwajima amezitaja changamoto zinazoathiri jitihada za utekelezaji wa mpango huo kuwa ni pamoja na  utendaji usioridhisha wa Kamati za Ulinzi wa Wanawake na Watoto hususan kwenye ngazi za Mamlaka za Serikali za Mitaa/vijiji.


“Utengaji na utolewaji duni wa fedha za utekelezaji wa afua za MTAKUWWA katika ngazi zote,ushirikiano mdogo wa kiushahidi kutoka kwa waathirika wa vitendo vya ukatili dhidi ya watuhumiwa hususan watu au ndugu wa karibu na hivyo kusababisha kesi nyingi kushindwa kutolewa maamuzi na watuhumiwa kuachiwa huru,”amesema


Ameitaja changamoto nyingine ni upungufu wa watendaji wa kada mbalimbali zinazohusika moja kwa moja katika kushughulikia masuala ya ukatili nchini kama vile Maafisa Ustawi wa Jamii, Maafisa Maendeleo ya Jamii, Polisi na Wanasheria hususan katika ngazi za kata na vijiji au mitaa.


“Uwepo wa mila na desturi zenye madhara ndani ya jamii zetu zikiwemo za ukeketaji na ndoa za utotoni ambazo zimeendelea kumkosesha haki za mtoto wa kike na kuathiri maendeleo na ustawi wake,”amesema.


Amesema mpango huo  una  lengo la kupunguza ukatili dhidi ya wanawake na watoto kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2021-22 ambapo, ili kufikia lengo hilo, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa Maendeleo imekuwa ikitekeleza afua mbalimbali zinazolenga kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto kupitia maeneo nane.


Waziri Gwajima amesema kamati za Ulinzi wa Wanawake na Watoto 18,186 zimeanzishwa ngazi ya Taifa, Mkoa, Halmashauri, Kata na Kijiji/Mtaa mwaka 2020/21 ikilinganishwa na 16,343 mwaka 2019/20, sawa na ongezeko la Kamati 1,843.


Amesema Madawati ya Jinsia na Watoto yameanzishwa katika Vituo vya Polisi ambapo hadi Desemba 2021 yalikuwa 423 na Madawati Matano (5)nya Jinsia (5) katika Taasisi za Elimu ya Juu na Kati.


Amesema huduma za msingi na hifadhi ya dharura kwa waathirika wa ukatili zimeendelea kutolewa katika nyumba salama 9 katika mikoa ya Arusha (2), Iringa (1), Kigoma (1), Mara (2), Manyara (1), Morogoro (1) na Mwanza (1).


Amesema jumla ya watoto 167 (wavulana 111 na wasichana 56) na wanawake 269 walipata huduma.


“Serikali imeendelea kuwawezesha kiuchumi wanawake, vijana pamoja na watu wenye ulemavu kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri,”amesema


Amesema  katika kipindi cha Julai 2020 hadi Aprili 2021, jumla ya mikopo (isiyo na riba) ya Tsh bilioni 27.07 ilitolewa kwa wanawake ikilinganishwa na Tsh bilioni 23.86 zilizotolewa mwaka 2019/20.


Kwa upande wake,Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum,Dk. Zainabu Chaula amesema jamii inajukumu la kufanya kila mmoja atimize wajibu wake katika mpango wa MTAKUWWA.


“Niwaombe MTAKUWWA  kila mtu atimize wajibu wake malezi ni jukumu letu sote hivyo ni lazima tusaidiane katika hili,kumekuwa na maombi mengi ofsini wengi wakitaka wapewe leseni kusajili makazi sasa hawa watoto wanatoka wapi na baada ya kufikisha miaka 17 wanafanya nini ? amehoji Naibu Katibu Mkuu huyo.


Naye,Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ambaye ni Afisa Kilimo Mkoa wa Dodoma,Benard Abraham  amesema suala la ukatili dhidi ya watoto na wanawake ni suala mtambuka ambapo amedai sababu kubwa inayosababisha ni kiwango cha uchumi kuanzia ngazi ya kaya.


“Kukiwa na uchumi nyumbani suala la ukatili linapungua hapa ni suala la kipato na uchumi kukiwa na kipato lazima ukatili upungue lakini kipato kikiwa kidogo kunakuwa na shida kidogo,”amesema.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI