Header Ads Widget

UMILIKI WA ARDHI WA WAYAO

 




Adeladius Makwega_Zanzibar


Matabaka katika umiliki wa ardhi kwa kabila la Wayao nayo yalikuwepo, kwani wale waliokuwa wakimiliki ardhi yenye rutuba na wale waliokuwa na ardhi yenye rutuba kiasi. Koo ambazo zilikuwa zinakaa katika ardhi yenye rutuba na kuzilimiki kabla ya wengine walipewa jina la Nakamo.


Koo hizi zilikuwa zinakaa huko Chitangali jirani na ukanda wa safu za miinuko ya Wamakonde ambayo ni eneo la Newala kwa sasa. Mara baada ya kifo cha chifu wao aliyefahamika kama Nakamo (II) Wakuu wa familia hiyo ya chifu walimteua ndugu mwingine kuchukua nafasi hiyo ya uchifu na kuwa Chifu Nakamo (III). Kipindi hiki wakati Chifu Nakamo III anakabidhiwa hawakuwa na wakati mzuri sana, kulikuwa na matukio mengi mabaya na ya kutisha, kwa maana hiyo haukuwa utawala wa amani.


Ulikuwa ni utawala uliomwaga damu nyingi za watu kutokana vita vya wenyewe kwa wenyewe, kwa upande wa Kusini wa Wayao hao. Chifu Nakamo (III) kuitafuta amani aliamua kuyahamisha makao yake makuu kutoka Chitangali kwenda Chiwata na akaweka makaazi yake katika eneo linalofahamika kama Ngatala, kwenye safu ya miinuko ya Umakonde.


Msomaji wangu tambua kuwa katika utawala wowote ule amani ni jambo la msingi sana, kama utawala hauna amani kila linalofanyika hata kama liwe jema linaweza kuonekana baya, lakini pia kwenye kumbukumbuku za watu baadaye doa la mabaya linaweza kuvuma zaidi ya yale mema yaliyotendeka.


Ukoo huu wa Chifu Nakamo waliweza kumiliki eneo kubwa la ardhi lenye rutuba na wakalipa jina la Chajila kwa Kiyao. Kwa watu wa koo zingine wasio na nasaba na chifu walifika hapo kufanya kazi kama vibarua wa Chifu Nakamo. Huku baadhi ya vibarua hao waliweza kufanya kazi vizuri kwa chifu waliweza kupewa vipande vya ardhi kwa kipindi fulani tu vya muda, muda ulipokwisha ardhi hiyo ilichukuliwa na Chifu Nakamo.


Jamii iliyomzunguka Chifu kama vibarua walitambua kuwa fulani alipewa ardhi kwa sababu mbalimbali ziwe zilizoweza kutamkwa au la, lakini walitambua hilo.


Hali hii iliendelea hadi Tanganyika ilipopata uhuru ambapo umiliki wa ardhi ulihamishwa kutoka kwa watu binafsi na sasa kuwa kwa serikali, mamlaka hayo kuwa ya Ndugu Rais kwa mujibu wa sheria zilizotungwa.


Sasa kila mmoja aliweza kutumia ardhi hiyo isipokuwa yale maeneo yaliyotengwa na serikali kwa matumizi maalumu. Bila kujali kama ilikuwa imilikiwa na chifu au nani hapo awali.


Jambo la kustajabisha japokuwa uhuru huo wa kutumia ardhi katika ukanda huo wa Wayao, wao waliendelea kuwaheshimu wale waliokuwa wakimililiki ardhi awali kama vile machifu.


Mtu alipokuwa akitaka kutumia ardhi hiyo alifunga safari hadi kwa koo hizo za uchifu na kuwasalimu na kuwaomba, jamani ehee mie naingia kukata kuni, jamani ehee mie naomba kulima kidogo, jamani ehee naenda kuokota hiki, jamani ehe mie naenda kuokota korosho.


Swali lililopo je kwanini Wayao walifanya hivyo? Jawabu lake ni kuwa jamii hii inaamini katika Ushirikina na Kulogana. Kuna uchawi mwanakwetu. 


“Hata kama serikali imeruhusu kutumia ardhi hiyo lazima mwenye mali wa asili moyo wake uridhie, bila ya mwenye mali wa asili kuridhia lazima yeye atafanya jambo au mizimu itakasirika na kulipiza kisasi.” Hii ilikuwa ndiyo imani ya Wayao.


Hawa jamaa ambao walikuwa wanamiliki ardhi awali kama machifu wanachokifanya wanapofuatwa, huwa wamekuwa na desturi ya kutoonesha majibu ya moja kwa moja ya ndiyo au hapana. Majibu hayo huwa ni mtego lakini huwa majibu ya hekima.


Hapo pia walikuwa wanajibu kupata usalama wao binafsi kuogopa kusumbuliwa na serikali kwamba sheria inasemaje na nyinyi mnafanya nini? Wengine wakiamni kuwa hata familia za kichifu zenyewe walihofiwa mizimu kuwakataza hilo na kuwageuka.

Mwanakwetu baadhi ya majibu ni haya:


“Enzi sya Chajila sipita, agambe kulima.” (A1)


Maana yake ni kuwa, muda wa sisi kumiliki ardhi umepita, wewe nenda kalime.


“Yajila ngapangwa ni usavi ngapangwa, agambe kutenda yakusaka.”(A2)


Muda wetu wa kumili ardhi umekwisha na muda wa kukuloga umekwisha, wewe fanya ufanyalo.


Ukitatazama majibu ya sentensi zote mbili A1 na A2 yote ni majibu yenye hila kwa hiyo yule aombaye hufanya hivyo kwa taadhari mno maana chifu huwa na silaha ya nguvu za ziada(ushirikina).


Msomaji wangu fahamu jambo moja kuwa majibu ya chifu ya sentensi A1 yana nafuu kuliko majibu ya A2.Pia msomaji wa matini haya fahamu kuwa kwa Wayao wamiliki wa ardhi wanaitwa Achinalukosyo na wafanyakazi wanaitwa Achikapolo. Achinalukosyo wanaweza kuwatania Achikapolo kwa kusema:


“Anyamwe wose mwaliji achikatumetuma vetu, nnjiseje ambano mumbanganyichisye masengo nne.”


Ikimaanisha kuwa wewe pamoja na ndugu zako mlikuwa wafanyakazi wa chifu wetu, rejeeni majukumu yenu mje mnitumikie.


Miaka 1970 serikali ilianzisha vijiji vya ujamaa ambapo watu walitakiwa kukaa pamoja na ndiyo maana kwa Wayao utakutana na vijiji kama vile Zingatia, Muungano, Namauya, Ngalinje, Mpangule, Chiwata Pansinde na Chiwata. Majina hayo ya vijiji yakilingana na zile harakati za kuanzishwa kwa vijiji hivyo.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI