Header Ads Widget

MAMA MWENYE BAIBUI NYEUSI

 




Adeladius Makwega_Dodoma


Januari 13, 2022 niliingia katika Boti ya Kilimanjaro inayomilikiwa na Azam Marines majira ya saa 10 47 alasiri na kuanza safari ya kurudi zangu Dar es Salaam. Kwa ratiba ya boti hiyo ilitakiwa kuondoka saa 10.30 kwa hiyo safari yetu ilikuwa nyuma kwa dakika 17.


Kwa kuwa nilikuwa katika daraja la makabwela nikivinjari na makabwela wezangu niliamua kukaa kiti cha mbele kabisa, katikati ya boti hii, abiria tulikuwa wengi mno huku wengine wakitoka kwa nje upande wa mbele wa boti, walikaa katika viti hivyo huku wakipunga upepo wa bahari.


Sehemu niliyokaa, nilikuwa na mama mmoja ambaye alioneka ni mtu mzima kiasi tunaweza kulingana kidogo, alikuwa amevalia baibui nyeusi huku akiwa na binti yake aliyevalia fulana nyeupe, suruali ya jinzi na miguuni akiwa amevalia mikufu, binti huyu nilimuona akiongozana na mtoto mdogo ambaye kwa mtazamo wangu alikuwa ni mtoto wake. Kwa hiyo mama mweye baibui nyeusi kama kunizidi basi yeye alikuwa ameshajukuu wakati mie bado. Siyo kwamba watoto wangu tasa au wagumba, la hasha bado wanasoma, mwanakwetu na mie nitajukuu tu


Safari ilianza vizuri kabisa huku mawimbi ya bahari yakiwa ya kawaida na jamaa wa boti hii walituelekeza namna ya kujiokoa pale ajali inapotokea. Niliyasikiliza kiumakini maelekezo hayo, nadhani abiria wengi hawakuwa makini kama nilivyokuwa mimi, kwani mimi mara ya mwisho kuogelea ilikuwa mwaka 1990 ambapo nilitembelea pwani ya Mtoni Kijichi Dar es Salaam.


Siyo kwamba mimi ni muoga wa maji, hapana, maana asili ya kwetu huko upogoroni kuna mto mkubwa unapita maji mengi unaitwa Mto Luhombero una maji safi, matamu, samaki wengi lakini kuna mamba wengi. Hata kama nina asili ya kuyaona maji lakini maji ya bahari ni maji mengi na ni maji ya chumvi, siwezi kujifanya mie jemedari baharini labda kidogo jemedari wa nchi kavu.


“Tahadhari, pale ajali inapotokea hakikisha usibebe mzigo wowote.” 

Hayo yalikuwa miongoni mwa maelekezo mengi ambayo yalikuwa yakielezwa na jamaa hawa wa boti hii. Hapo nilibaini kuwa kumbe inapotokea ajali jambo la msingi ni kuhakikisha kuwa uhai unaokelewa siyo fedha, dhahabu au lulu.


Maelekezo hayo yalipokamilika hawa jamaa wa boti hii walituweka picha moja ya kutisha sana ambayo ilikuwa ikiwaonesha mijusi wakubwa waliokuwa wakipambana na binadamu. Sikuelewa kisa cha binadamu hao cha kupambana na mijusi hao. Binafsi ni muda mrefu sana sijakaa na kuangalia filamu, nakumbuka filamu yangu ya kwanza na ya mwisho ni Coming to America ambayo nilitazama miaka mingi iliyopita. Filamu ya leo na mijusi vitani ndiyo ilinichefua zaidi.


Picha hii ilikuwa inatisha mno kwa hiyo ilikutoitazama mno nilijaribu kuutafuta usingizi wa lazima angalau nisiitazame. Ukiwa katika usafiri wa umma abiria hauna nafasi ya kuchagua cha kuona wala cha kusikiliza. Macho na masikio yanakutana na vyote tu.


Niliyafumba macho yangu alafu nikauchukua mkono wangu wa kushoto na kuziba macho yangu. Nikiwa nimeyaziba macho yangu nilikilaza kichwa changu katika kiti cha boti hii huku safari ikiendelea vizuri. Kwa kufanya hivi mwanakwetu niliziba macho na siyo masikio. Kwa hiyo kandoni masikio yangu yalikaribishwa na milio ya injini ya boti hii ambayo ilikuwa sawa na kinanda kwa mtu anayeutafuta usingizi huo.


Masikio yangu yalikuwa yakisikia kelele tano kwanza za runinga ya boti hii, Pili milio ya injini ya boti, tatu sauti za wafanyabiashara ndogo ndogo ndani ya boti, nne sauti za abiria wezangu na tano sauti za simu wanazopokea abiria wezangu.


Sasa tulikuwa tayari tumetumia zaidi ya dakika 30 katika boti hii. Mama jirani yangu aliipokea simu yake huku akiongea na mtu ambaye yu Dar es Salaam.


“Mimi nipo katika boti… Eh mgonjwa anaendeleaje?... Nadhani kama tutawahi nitapitia moja kwa moja Muhimbili tuje kumuona…Nipo naye na mwanawe… Sawa hakuna neno… Inshalaaaa! ”


Japokuwa nilikuwa nimeyafumba macho yangu na kelele zote hizo nne sikuzisikia, yaani za runinga, milio ya injini ya boti, sauti za wafanyabiashara ndogo ndogo wa bidhaa ndani ya boti, na sauti za abiria wezangu lakini sauti ya tano ya simu wanazopokea abiria wezangu hasa ya huyu mama, ilinifanya niwe makini, nikifuatilia irabu na silabi ya maongezi yake.


Mama huyu kwa kuwa alikuwa jirani yangu, kuna wakati usingizi ulikuwa ukinipitia, basi nilikuwa namuegemeaegemia kwa bahati mbaya, kwa hiyo tulikuwa tumekaa vizuri huku nayeye mara usingizi ukimpata nayeye alikuwa akiniegemeaegemia.


Natambua msomaji wa matini hii unaweza kuona wivu namna nilivokuwa namuegemea mama huyu na yeye alivyokuwa ananiegemia, hivyo ni vitu vya kawaida sana katika vyombo vya usafiri iwe basi, meli na hata ndege ndiyo maana waswahili wanasema msafiri kafiri.


Kwa kuwa tulikuwa jirani na tumezoena vizuri katika safari hii, nilimuuliza habari za mgonjwa huyo aliyelazwa Muhimbili? Alinijibu ndiyo amelazwa Muhimbili kwa kuwa ana mkewe bara nayeye ni mkewe wa Zanzibar. Nikampa pole sana kwa kuuguza mumewe, huku akiniambia huyo aliyekuwa akiongea naye ni mke mwezake.


Kumbuka tu msomaji wangu tupo katika boti tunaelekea Dar es Salaam. Nilibaini kuwa sasa mgonjwa wa Zanzibar anaweza kutibiwa Bara kwa kuwa ni Mtanzania, akija bara siyo mgeni. Nilipata wasaa mkubwa wa kutafakari hilo la mume wa mama huyu, nilikumbuka kuwa siku moja iliyotangulia kulifanyika kumbukumbu ya miaka 58 ya Mapinduzi ya Zanzibar.


Kwa kuwa niliyafuatilia maadhimisho ya mapinduzi hayo katika runinga, niliona namna vikosi kadhaa vya ulinzi na usalama vilivyoonesha ukakamavu na uhodari wao. Binafsi niliibaini jambo moja kubwa sana la nafasi ya Mzanzibari katika Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.


Pia nikiwa botini nilibaini kuwa Sultan Jamshid Bin Abdulla alikuwa hai na ametimiza miaka 92 na kwa hakika akiyafuatilia maadhimisho ya miaka 58 ya Mapinduzi ya Matukufu ya Zanzibar. Nikajiuliza swali hivi kama huyo Sultan Jamshidi Bin Abdulla kama amaejaliwa kuyafuatilia haya maadhimisho yetu ya mapinduzi, jambo gani linaweza kuwa tulimlingishia?


Mwanakwetu nipo botini natafakari hayo kwa swali hilo, Je mitutu ya bunduki? Je mizinga? Je makomandoo waliopita kwa ukakamavu katika viwanja hivyo? Je namna askari wetu walivyokuwa wakipiga gwaride? Je namna wananchi walivyojitokeza kwa wingi na kuujaza uwanja ? Au namna viongozi wetu walivyojaza Jukwaa Kuu? 


Je hivyo vyote nilivyovitaja enzi ya Sultan Jamshidi havikuwepo? Kwa hakika vilikuwepo.


Binafsi nilibaini kuwapo kwa jambo moja kubwa sana ambalo Sultan Jamshid Bin Abdulla litakuwa linamkereketa mno, nalo ni nafasi ya Mzanzibari katika muungano. Kwa sasa uwepo wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, mzaliwa wa Zanzibar. 


Zanzibar chini ya Sultan Jamshidi miaka 58 nyuma jambo hilo lingekuwa Nyota ya Jaha kufanyika. Kwa hakika mapinduzi ya mwaka huu tumemlingishia mno Sultan ambapo wakati huo ilikuwa ni ngumu kutokea kwnai Zanzibar ilikuwa chini ya mtu mmoja ambaye ni Sultan.


La msingi kwa sasa ni maboresho ya maisha ya Watanzania kwa udi na uvumba kwa ajili ya ustawi wa maisha ya binadamu.


Nikiwa natafakari haya moyoni, mama mwenye baibui nyeusi akasema shekhe amka! Tumeshafika forodhani. Kweli niliamka nakumshukuru mama huyu, nilijitwika begi langu mgongoni na mie kushuka botini.


Nilitoka botini na nilipofika Sokoine Drive nilikunywa kikombe cha kahawa na kashata moja angalau kuondoa uchovu wa safari hiyo na baadaye kuanza safari ya kuelekea kwetu, Mbagala.


makwadeladius@gmail.com

0717649257

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI