Header Ads Widget

KUTOKA BARA KWENDA VISIWANI

 




Adeladius Makwega

Zanzibar.


Nikiwa Dar es Salaam niliwauliza ndugu zangu juu ya safari yangu ya Zanzibar, waliniambia Januari 12, 2022 ni siku ya Mapinduzi ya Zanzibar kutakuwa na watu wengi sana na safari itakuwa ngumu. Hata vyumba vya kulala huko vitakuwa ghali, ili kuondoa usumbufu walishauri nisafiri Januari 13, 2022. Nikate tiketi ya kwenda na kurudi kwani usafiri utakuwa mgumu kutokana na fainali ya Kombe la Mapinduzi baina ya Simba na Azam.


Kweli niliweka nafasi ya kwenda na kurudi kwa nambari 18890104 yenye ufunguo ETWD kwa boti ya saa 1.00 asubuhi saa 2.30 nitakuwa Zanzibar na iwavyo na iwe saa 10.30 jioni nitapanda boti ya kufika Dar es Salaam 12.30 jioni kwa majaliwa ya Mungu.


Nilijulishwa kuwa natakiwa kulipa 50,000/ ambapo 25,000 kwenda na kiasi hicho ni cha kurudi. Kampuni hii ya boti waliniambia kuwa natakiwa kulipa kiasi hicho saa tatu kabla ya muda wa safari. 


Nilifika Sokoine Drive muda uliotakiwa na kulipia tiketi zangu za kwenda na kurudi Zanzibar na ilipofika saa 1 kamili boti iling’oa nanga.


Nikiwa katika boti hii kwa mbali niliona sura kama za nyumbani kwetu, dada mwenye macho makubwa, mweusi hivi, mrefu, mwenye miguu ya bia na kichwa chake kikipambwa na rasta zilizosukwa katika mtindo wa Bob.


Nilimsogelea na kumwambia kidumu Chama Cha Mapinduzi, alijibu kidumu. Huyu alikuwa ni Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya mojawapo Jijini Dar es Salaam.


Nilimkumbatia, nikamlaki, kumalizia na busu, huku abiria mmoja mkono wangu wa kushoto akiona gere utadhani nilimkumbatia mkewe.


Alinisalimu kaka kwema? haya Zanzibar unafuata nini? Umepata mke mwenzangu wa Kipemba? Nilicheka tu, na mimi nikamuuliza na wewe una babu wa Kiunguja? Binamu yangu alicheka tu akisema yeye amtoe wapi? Alinituhumu kwa kumkataa na kwenda kuoa Usambaani.


Nilitafuta upenyo wa kuketi na binamu yangu huyu, upenyo ulipatikana, tuliyazungumza mambo mengi ya kifamilia na kuyamaliza. Binamu yangu huyu kwa kuwa ni mwanasiasa nilitumia upenyo huo kumuuliza maswali kadhaa juu ya chama hiki kikongwe Barani Afrika.


Kumbuka tupo katika boti hii tunaelekea Zanzibar, huku mandhari ya bahari ikiwa nzuri na tukiona samaki wakiruka huku na kule na abiria wanzangu wakiwa kimya na sauti iliyokuwa ikivuma ni milio ya injini za boti tu.


Swali langu la mwisho kwa binamu yangu huyu Mpogolo/Mngoni kati ya maswali 39 lilikuwa hali ilivyokuwa katika Mkutano Mkuu wa CCM uliomchagua Mwenyekiti wa CCM mpya mwaka 2021 baada ya msiba wa Ndugu Magufuli.


Anasema kuwa walitoka Dar es Salaam pamoja na wajumbe wengine huku katika basi lao wakiwa na hali ya simanzi mara baada ya kifo cha Marehemu John Magufuli. Walipokuwa wanakaribia Dodoma walikaribishwa na mandhari ya Soko la Job Ndugai huku wajumbe wa mkutano huo wanaotokea Dar es salaam, baadhi yao wakitokwa na machozi na kubembelezana.


Walienda mbele kidogo walikutana na Kituo cha Mabasi yaendayo mikoani ambacho pia nacho kilijengwa na Magufuli, hapo simanzi iliongezeka kana kwamba ndiyo kwanza wanaenda Chato kumzika Magufuli, wakati maziko yalikuwa yameshafanyika.


Walipofika katika mkutano huo wajumbe wa CCM ambao walitokea Mwanza, Geita, Shinyanga, Tabora na Kigoma nao wakiwa na huzuni kubwa. Binamu anasema kuwa siyo kwamba wajumbe wengine hawakuwa na simanzi bali yeye aliwatazama zaidi wajumbe wa mikoa hiyo.


“Yaani kaka walikuwa wakiingia ukumbini pamoja, katika vikundi vikundi na kutoka hivyo hivyo. Kaka nilibaini kuwa japokuwa Watanzania tulikuwa tumempoteza rais wetu lakini Wasukuma na Wanyamwezi walikuwa wamempoteza ndugu yao.” Niliambiwa na binamu.


Chama kilitupangia vyumba, huku mbunge wetu alikuja na kutusalimu, akisema jamani mbona wanyonge sana, mbona siyo kawaida yenu kuwa hivyo? Mbunge huyu alijibiwa kuwa tumempoteza rais na mwenyekiti wa chama chetu. Mbunge huyo alitukabidhi kila tulikuwepo hapo kiasi cha shilingi 20,000/-lakini fedha hiyo haikubadilisha hali yetu ilikuwa sawa na kumpa mkono mfiwa na kumuacha aendelea kumkumbuka nduguye aliyefariki.


Kura zilipigwa za kumthibitisha mwenyekiti huyo mpya wa CCM taifa, kabla ya wajumbe kupiga kura mmojawapo wa Wenyeviti wa CCM taifa mstaafu alizungumza mengi juu ya uchaguzi huo, shabaha ilikuwa kupita salama katika kipindi hicho kigumu. Kura zilipigwa na kuhesabiwa na matokeo kutangazwa na shabaha ya CCM kupita salama katika kipindi hicho iliweza kuyameza matokeo yaliyotangazwa.


Binamu yangu huyu aliingia msalani na kuniacha pahala tulipokaa, na mie kutumia wasaa huo kuinua kichwa changu juu na kutazama runinga ambayo ilikuwa usoni kwetu katika boti hii.


Macho yangu yalikaribishwa na picha ya gari linalotembea barabarani, likifunguliwa geti na mabinti wakicheza wimbo kama singeli hivi, wachezaji hao walivalia nguo za rangi nyekundu, nyeupe na nyeusi, wakinyanyua vidole juu.


“Yamenifika kwako, Kumbe mwanamke mwezangu, Bwana wako kalalamika, 

Kila akija nyumbani, Ati haujui kupika, Kula kwako hatamani

Kwangu kalipenda tembele, Tena laini laini, Shoga umenyimwa upole, Tajiri wa kisilani

Naa samahani ah samahani, Mwanzo sikujitambulisha, Mimi naniii, 

Mie ni mke mwenzio, aka Nyumba ndogo,Tena nimemganda mumeo, 

Kama kichwa na kisogo,Sina ubayaaa, Sina ubaya nawe, ukinichukia, Sina ubaya nawe, Sina ubayaa, Sina ubaya nawe, Ukinichukia unanionea bure….”


Binamu aliporudi, alinigusa begani akaniambia naona unamtazama Zuhura Othman Soud (Zuchu), nikasema kumbe huyu ndiye Zuchuu? Alinijibu kuwa ndiyo, tena ni binti wa Hadija Kopa. Nikamjibu mimi namfahamu marehemu Omary Kopa. Binamu alinijibu kuwa Omari Kopa ni mambo ya zamani. Zuchu ndiyo habari ya mjini na huo wimbo unaitwa Nyumba Ndogo.


Binamu aliniuliza kama huyo Omari Kopa unazikumbuka nyimbo zake? Nilimjibu nazikumbuka vizuri:Mpenzi Wangu Nipepe, Nifagilieni, Nadekezwa na Sitaki Ushambenga.


Binamu alijibu kuwa kweli unazifahamu, mara niliisikia honi ya botii ikilia poooooooo, kumbe ndiyo tulikuwa tunaingia Zanzibar, boti ilitia nanga.


“Nasema, Amasha zungusha, Wee zungushaaa, Sasa Wanjala zungusha,

We zungusha, Hadija Kopa zungusha, Mama Dangote zungusha…”


Wimbo huo uliendelea kutusindikiza abiria tuliokuwa tunashuka na mie nilibeba begi langu begani kuelekea huko niendapo na binamu kuelekea aendapo.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI