Na WAMJW-DOM
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Dorothy Gwajima ametoa wito kwa Makatibu Wakuu wa Wizara za Kisekta, Wakuu wa Mikoa na Mashirika yasiyo Yakiserikali hapa nchini kuwajengea uwezo watendaji ngazi ya Halmashauri na Wilaya ili kuwezesha ufanisi wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya awali ya Mtoto.
Dkt.Gwajima ametoa wito huo leo Desemba 13 2021, jijini Dodoma wakati akizindua programu hiyo ya kihistoria na ya kwanza Afrika Mashariki na Kati huku lengo likiwa kukabiliana na changamoto ya makuzi ya watoto chini ya miaka nane ikiwemo wimbi la kuongezeka kwa ukatili na idadi kubwa ya vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano kutokana na lishe duni kila mwaka.
DKt Gwajima amesema, takwimu za mwaka 2018 zilibaini zaidi ya watoto 2,600,000 chini ya miaka mitano wamedumaa na kwamba asilimia 43 ya watoto wapo kwenye hatari ya kutofikia hatua timilifu ya ukuaji na maendeleo yao kutokana na viashiria mbalimbali vikiwemo utapiamlo na unyanyasaji wa watoto.
"Takwimu za mwaka 2018 zilibaini zaidi ya watoto 2,600,000 chini ya mika mitano wamedumaa na kwamba asilimia 43 ya watoto wapo kwenye hatari ya kutofikia hatua timilifu ya ukuaji na maendeleo yao kutokana na viashiria mbalimbali vikiwemo utapiamlo, kukosekana kwa uhakika wa chakula, msongo wa mawazo katika familia, miundombinu duni katika familia, na unyanyasaji wa watoto." Amesema.
Wazazi na walezi kutokuwa karibu na watoto kunachangiwa kwa kiasi kikubwa kukosekana kwa uelewa wa kina kuhusu Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto. Alisisitiza Dkt. Gwajima.
Aidha, Dkt Gwajima amesema kuwa, Serikali inatarajia kujenga vituo vya mfano vya kijamii vya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto katika kila kijiji/mtaa na kwenye shule za msingi nchi nzima ili kukabiliana na changamoto ya ukatili na udumavu nchini.
Uzinduzi wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya awali ya Mtoto umefanyika leo Desemba 13, 2021 katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Mawaziri, Waganga wakuu wa Mikoa, Maafisa Ustawi wa Jamii, Waandishi wa Habari Wabobezi, Makundi Maalum ya Watoto na Mashirika ya Kimataifa.
0 Comments