ADELADIUS MAKWEGA
MBAGALA.
Kabila la Wachaga ni miongoni mwa makabila yenye utani miongoni mwao na makabila jirani yao. Neno hilo la utani kwa wachaga kwa asili lilikuwa linayahusisha maneno kama Shitalue, Irumana na Inyere ambayo inaaminika kuwa kwa sasa ndani ya kichaga maneno haya yameshapotea. Kwa wachaga kwa sasa neno linalomaanisha utani ni ni Kitalue na wingi wake ni Shitalue likiwa na asili ya neno taluo ambalo linamaanisha utani.
Kwa hawa jamaa utani umegawanyika katika namna kadhaa kwanza utani wa ndani ya familia, utani wa koo na koo, utani wa chifi na chifu na utani baina ya watu wengine. Mfano watu dhidi wezi, kati ya matajiri na wale wachoyo, utani katika ngoma na utani misibani.
Kwa utani katika familia upo baina ya dada na mke wa kaka yake wifi na wifiwe. Binti aliyeolewa huwa ni mgeni kwenye hii familia mpya kwa hiyo yeye huwa anapewa rafiki yake wa karibu ambaye na dada wa bwana harusi. Dada wa bwana harusi anaitwa moli na bibi harusi kwa wifi yake anaitwa mpora.(moli na mpora)
Kwa wachaga bibi harusi ambaye ameolewa na hana utani na wifi zake huyo utambulika kama ni binti ambaye ameshindwa kutimiza wajibu wake ipasavyo. Huyu uonekana kuwa wa kupewa talaka tu. Hapo kuna sentensi kama hii. Moli kyelya omkore kyokwi? Akimaanisha tayari umeshanipikia chakula changu? Na majibu yake huwa Eeeh mii oko akimaanisha ndiyo mume wangu.
Utani huu ufikia pahala hadi bibi harusi umjibu wifi yake kuwa unadai chakula mbona haujaleta pesa ya chakula hicho?Tambua kuwa hapa utani utakuwa umepamba moto
Pia upo utani baina ya mama wa bwana harusi na bibi harusi mwenyewe, hapa nia ya utani ni kumpa nafasi bibi harusi kujua kuwa sasa amepata mama mwingine wa kweli. Kama mama yake mzazi wa kule alipotoka/ alipozaliwa. Hapo usaidia bibi harusi kujisikia vizuri katika makaazi mapya. Mama huyu anaweza kusema kuwa anyi nacho alengendie mpora alaichi manya mamii wai?
Akimaanisha nani huyu aliyeniletea bibi harusi ambaye hampendi mama aliyemzaa bwana harusi? Maneno haya huwa ni makali sana lakini bibi harusi anaweza akajibu atakavyo kama vile Naacho akundi mamii alaichi moli mana oke akimaanisha ni mama huyu huyu ambaye hampendi mke wa mtoto wake. Utani huu unasaidia sana kuweza kuishi vizuri kwa pamoja bila migogoro kwani wakati mwingine hata jambo zito husemwa kwa utani lakini ujumbe huwa umefika tayari.
Pia wachaga wana utani baina na mke wa mjomba na mtoto wa dada wa mjomba. Nyi kiki mosingana cha mka omjomba na mho? Kwanini mnagombana sana kama mtu na mke wa mjomba wake? Maneno haya yanaweza kumfanya mtu mchoyo kuacha tabia hizo kwa lugha ya utani , kuacha tabia zozote mbaya na kumbadilisha tabia ndugu huyu.
Utani mwingine mpwa anaweza akapika pombe kwa wajomba zake akawaandalia pombe hiyo ya mbege na wakati wanakunywa anaweza kusema waho wako iha kanyi konyu, orio mfiri kuchienyi kuwore mndu ochimfuna pfo akimamanisha kuwa. Wajomba zangu hapa kila siku ni kwenu na hakuna atakayewafukuza.
Pia kuna utani katika ngoma za asili za kichaga hasa kwa vijana huwa kunawakati kunakuwa na ngoma ambayo huwakutanisha vijana wengi wa kike kwa wakiume hapo mtu anaweza akapokonywa mpenzi wake na mtu mwingine kuondoka naye kwa nguvu. Katika ngoma hiyo matusi na ugomvi ni jambo la kawaida na hakuna kushitaki baadaye binti huyo wazazi watajulishwa kuwa yupo kwa ukoo fulani.
Katika ngoma hiyo maneno ya dharau na vijembe hutamkwa dhidi ya mwanamme anayetaka kuporwa msichana wake kwa mfano Ndeichp nururo,aloi mndu cha alekuruo nyi na mndu? Akimaanisha kuwa nimesikia kuwa kuna mtu anataka kukuoa kweli mtu huyo anayo hadhi ya kukuoa wewe?
Wachaga pia wanao utani katika koo zao, hapa natanguliza samahani kama mtu ukoo wake utatajwa katika namna mbaya asichukie nia ni kutoa,elimu ya utani tu.
Ukoo wa Makundi ulitazamwa kama ukoo ambao haukuwahi kupigana vita vyovyote kazi yao kubwa ni wafua vyuma tu na kazi zote zinazohusika na nyundo ambao kwa kichaga ni nyundo ni Kiria. Huku wakipewa jina lingine ngache yaani fahari .Ukoo wa Minja hawa walitazamwa kama wachawi na walozi mtu yoyote mchawi kwa wachaga walimuita Mkominja yaani wa ukoo wa minja.Ukoo wa Mrema hawa walitazamwa kuwa ni watu wenye sauti kubwa yenye mikwaruzo au wako kipferepfere.
Huku kukiwa na utani baina ya chifu na chifu jambo hili ni matokeo ya machifu hao kuingia vitani na mara baada ya chifu mmoja kushindwa basi walianza kuitana majina mabaya.
Utani wa mwanzo ulikuwa baina ya chifu wa Mamba na chifu Marangu. Wachaga wa Mamba mara zote wapo mashariki mwa Marangu na huwa watu wa Mamba wanapokwenda kwao wanapita Marangu. Sasa hawa Wamamba wanapopita kwa Wamarangu huwa wanasema kuwa Akiliya Kimakuna kiheri icha, ikimaanisha kuwa mwanamke ambaye ni miongoni mwa koo za Moshi nayeye anakuja. Na wakati mwingine husema kuwa Kimangi kyanyu kishimbi nguchu wakimaanisha kuwa chifu wao ana mabusha / matende.
Utani wa wachaga upo pia kwa makabila mengine mathalani Wapare kwa wachaga wa Vunjo, Mwika, Mamba na Marangu hawa wanawatazama Wapare kwa namna nyingine. Mpare akiwaona hawa huwa kabla ya kusema nao neno lazima atatema mate chini kuonyesha dhihaka. Kwa hawa jamaa pia wakimuona Mpare muda mwingine wanaweza hata wakalalua mavazi yao kwa dharau.
Kwa kifupi hao ndiyo Wachaga na utani miongoni mwa wao kwa wao na makabila mengine. Mwanakwetu kama umeolewa na wachaga alafu hauna utani na wifi yako na mama mkwe tambua kuwa taraka ipo njiani inakuja. Kwa leo niishie hapo, nakutakia siku njema.
makwadeladius@gmail.com
0717649257
0 Comments