Mkuu wa mkoa wa Arusha John Mongela amesema serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za bodi ya ununu na ugavi zinazolenga kupunguza au kuondoa kabisa uzembe na ukiukwaji wa maadili katika fani ya ununuzi na ugavi kwani pesa nyingi za serikali zinatumika kupitia taaluma hiyo.
Mongela aliyasema hayo wakati akifungua kongamano la 12 la la wataalamu wa ununuzi na ugavi kwa niaba ya waziri wa fedha DkT Mwigulu Nchemba ambapo alisema kuwa bado kuna wataalamu wachache wanafanya kazi chini ya kiwango cha taaluma yao na kuagiza bodi ya PSPTB kuendelea kusimamia taalumu hiyo kwa kuchukua hatua mathubuti kuinua weledi wa wataalamu pamoja na wengine wote wanaoshiriki katika mchakato wa ununuzi na ugavi kwa kuwajengea uwezo katika taratibu za manunuzi na usimamizi wa mikataba .
Alisema kuwa mada walioiweka katika kongamano hilo ambayo inasema kuwa “ubunifu wenye suluhisho katika utekelezaji wa mnyororo wa ununuzi na ugavi kwa kutambua ushindani na mapinduzi ya viwanda kwa maendeleo ya jamii ambapo alibainisha kuwa mada hiyo itaipa changamoto bodi ya PSPTB na wataalam kuweza kutambua umuhimu wao katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa na serikali ili kuweza kuongeza tija na faida katika sekta binafsi .
Aidha alisema kuwa waendelee kuchukuwa hatua madhubuti kwa mtaalamu yeyote anaekiuka kanuni za maadili au kutoa ushauri wa ununuzi kinyume na sheria ya ununuzi wa uma bila uwoga wowote kwani uzembe na ukosefu wa weledi katika kusimamia mnyororo wa ununuzi na ugavi unapelekea kukwamisha utekelezaji wa miradi pamoja na miradi mingi kufanyika chini ya kiwango.
Alisema kuwa kuwepo kwa ukiukwaji mkubwa wa maadili kwenye kada hii iwe chachu ya bodi kuongeza usimamizi wa maadili na kuchukuwa hatua stahiki kwa wahusika kwani taaluma hii ni muhimu sana ili kufikia adhima ya serikali ya awamu ya sita ya kuendelea kuwaletea watanzania maendeleo kwa kasi .
Alitoa wito kwa waajiri wote kutoa ushirikiano kwa bodi haswa linapokuja swala la usimamizi wa taaluma ya ununuzi na ugavi pamoja kuzingatia matakwa yote na sheria za bodi ili kuleta tija ya miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali.
Alisema kuwa katika taasisi nunuzi 85 zilizofanyiwa ukaguzi kwenye viashiria vya rushwa miradi mitatu yenye kiasi cha shilingi milioni mia sita kumi na sita nukta tano ilibainika kuwa na viashiria vikubwa vya rushwa ukilinganisha na taarifa ya mwaka 2018\2019 iliobainika kuwa ukaguzi wa miradi 131 ulionyesha kuwa na miradi 39 ilikuwa na viashiria vya rushwa .
Kwa mujibu wa ukaguzi uliofanywa na mamlaka ya uthibiti wa manunuzi ya uma (PPRA) kwa mwaka wa fedha 2020/2021 umethibitisha kuwa ukaguzi wa mikataba 282 yenye dhamani ya shilingi za kitanzania bilioni elfu tano nukta saba na mikataba 281 sawa na asilimia 99.6 imesimamiwa vizuri na kuleta dhamani ya fedha huku mkataba mmoja ulionyesha kuwa na usimamizi wa kiwango cha chini sana .
Kwa upande wake mwenyekiti wa bodi wa ununuzi na ugavi (PSPTB)Jacob Kibona alisema kuwa atahakikisha anasimamia vyema taaluma na maadili ya taaluma ya ununuzi na ugavi ili kuwezesha taifa kupata dhamani ya kiasi cha pesa kinachoendana na manunuzi yaliotumika.
Alisema kuwa atafanya kazi kwa weledi uliotukuka kwa kipindi chote cha nafasi yake na kumaliza matatizo yote ambapo bodi itahakikisha inachukuwa hatua kali za kinidhamu kwa wataalumu wote watakao sababisha watu kupoteza imani na taasisi hiyo ya ununuzi na ugavi.
Naye mkurugenzi mtendaji wa bodi ya PSPTB Godfred Mbayi alisema kuwa kwa mwaka 2021 imesajili jumla ya wataalam 1166 ambapo wamefanya mitiani katika hatua tatu bila kutangaza kutokana na kutokuwa na bodi ya wakurugenzi na idadi hiyo imefanya idadi ya wataalamu kuongezeka na kufikia zaidi ya wataalam elfu 12000.
0 Comments