Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, amesema Serikali itaweka mfumo rafiki utakaosaidia kuleta uhusiano mzuri baina ya wamiliki wa mabasi na LATRA, Ili zikitokea changamoto za kiutendaji wazitatue kupitia mfumo bora zaidi.Mwandishi Fatma Ally MDTV Dar es Salaam
Aidha, amesema, mfumo wa Tiketi Mtandao, utaanza kutumika rasmi Aprili, mwakani, baada ya kupatiwa ufumbuzi kwa changamoto mbalimbali zilizolalamikiwa na wadau wa sekta hiyo, ambapo wamekubaliana kuna baadhi ya mambo yanahitaji mabadiliko ya sheria na kanuni.
Kauli hiyo, ameitoa jijini Dar es Salaam Disemba,20, 2021 katika kikao maalumu cha kupokea taarifa ya kamati ndogo iliyoundwa Julai, mwaka huu, kubainisha changamoto za mfumo wa Tiketi Mtandao na kupendekeza jinsi ya kuzitatua.
"Tutakaa Wizara, Wamiliki wa Mabasi (TABOA), Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) na Wizara ya Fedha na Mipango na tutayachakata maoni hayo yaliyopendekezwa yarekebishwe na tutayafanyia kazi, marekebisho mengine yatahitaji kwenda bungeni,"amesema Naibu Waziri Waitara.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kamati hiyo, ambae pia ni Mkurugenzi wa Huduma za Uchukuzi wa Wizara hiyo, Mhandisi Aron Kisaka, amesema kamati hiyo ilikuwa na wajumbe 11 ambapo changamoto 17 wamezifanyia kazi na taarifa rasmi wameiwasilisha kwa Naibu Waziri huyo ambapo imejadiliwa na kubainika kwamba kuna umuhimu wa kufanyika maboresho ya kisheria na yapo maeneo mengine yanahitaji kufanyiwa kazi na wadau.
"Julai, mwaka huu, Katibu Mkuu wa Uchukuzi aliunda kamati ndogo ya kuainisha changamoto zinazowapata wamiliki wa mabasi katika matumizi ya Tiketi Mtandao na baadaye kutoa ushauri wa namna ya kuzitatua"amesema Mhandisi Kisaka.
Amesema kuwa, kupitia kamati hiyo pia ilibaini wamiliki hawapati fedha zao, wakati abiria wanapokata tiketi, hivyo mfumo wa mtandao kuwa chini na maeneo mengine tiketi hazipatikani na changamoto zingine ambazo wamezibainisha.
Ameongeza kuwa kamati hiyo imekubaliana kurudi kufanyia kazi maeneo machache ambayo bado ni changamoto kwa wamiliki wa mabasi kwa lengo la mfumo huo kuanza kutumika Aprili, mwakani.





0 Comments