Adeladius Makwega
Itewe Mbeya.
Tulianza safari yetu majira ya saa tatu ya asubuhi na kutelemka milima kadhaa kutokea Mbeya Mjini. Baada ya dakika kama 37 tulifika katika Kijiji cha Itewe ambacho nilijulishwa kuwa kipo katika Wilaya ya Mbeya Vijijini katika Mkoa wa Mbeya
Katika gari hili tulikuwapo watu wanne, Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini ndugu Ado Komba(Mgoni), Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Ndugu John Mapepele (Mbena+Mnyalukolo), Dereva wa gari hilo la serikali Ndugu Johaness Kaimukirwa (Mhaya) na mie Mwana wa Kabwela(Mpogoro).
Tukiwa Itewe, Johaness Kaimukirwa alivutiwa na ndizi zilizokuwa zinauzwa barabarani na kuuliza Je! jamani mnanunua ndizi? Kweli wezangu waliitikia wito huo ambao ulihamasishwa na rubani wetu, nadhani kwa kuwa Wahaya ni wapenzi sana wa kula ndizi.
Tulikaribishwa na kundi la akinamama kadhaa wanaouza ndizi, viazi na maharage huku kila mmoja wetu kuelekea upande wake. Binafsi sikuwa na nia ya kununua chochote, nilikuwa nasoma ramani ya kijiji hichi huku wezangu wakifanya manunuzi kama bakishishi na posho kwa familia zao tuendako.
Niliamua kusogea jirani na mama mmoja ambaye alikuwa akiuza ndizi .
“Mama Tuma nitafutie mkungu mzuri wa ndizi unaofanana na uzuri wako, uwe wa shilingi 6,000/-”
Kijana mmoja aliyekuwa sasa anamkaribia muuzaji wa ndizi jirani yangu alitamka maneno hayo.
Binafsi nilivutiwa na maneno yake na nilimsogelea Mama Tuma(Msafwa) ili na mimi niuone huo uzuri wa mwanamke huyu. Nilipiga hatua ya kwanza, ya pili na ya tatu na akili yangu ilikumbuka juu ya Abigaeli ambaye Bibilia inamtambua kuwa alikuwa mke wa Mfalme Daudi aliyekuwa mzuri.
Uzuri wa Abigaeli ulijengwa katika mambo matatu kwanza urembo, pili akili na tatu utii. Hatua yangu ya nne ilinipa hamu ya kujua siri ya kijana huyu kumsifia Mama Tuma wa Itewe ni nini?
Mama Tuma alimpatia ndizi kijana huyo na kumuita kijana na kumbebea mteja wake na kuondoka zake huku akinikaribisha na kusema karibu, tuna ndizi za Malindi(tunda na kupika), Bukoba(kupika), Mzuzu(kupika) na Kisukari(tunda). Maelezo ya mama Tuma yalinivutia sana kwa kuifahamu ndizi ya Malindi ambayo inafanya kazi mbili kama tunda pale inapoiva na inapikwa pia. Maana kwetu chakula kikubwa ni wali tu.
“Malindi hautupi kitu, unaweza kuivundika lakini wakati unasubiri iive unaweza kuipika na kula kidogo kidogo.”
Nilimuuliza Mama Tuma namna ya kuivundika Malindi.
“Zipange vizuri katika sehemu yenye utulivu, unachukua maparachichi ya kienyeji, unayakata vipande viwili, unayaweka pembeni ya ndizi hizo na juu yake alafu unafunika kwa viloba na baada ya muda siku chache zitakuwa zimeiva vizuri tena zinakuwa za rangi ya njano itakayomvutia mteja.” Mama Tuma alisema.
Sisi hapa tunalima mpunga, hatulimi ndizi, hizi tunazipokea kutoka Tukuyu kwa kuwa huko zinapatikana mwaka mzima.
Kweli nilitoa pesa yangu mfukoni na kumpa Mama Tuma na kununua mkungu wa Malindi kwa shilingi 6,000/. Huwa nasafirisha mizigo hadi mikoa mingine kama mtu anahitaji nampatia, Mama Tuma aliniambia pia.
“Kazi hii hii inanipatia kipato changu cha kula mimi na familia yangu na maisha yanaenda vizuri sana.”
Nilibebewa mkungu wangu hadi kwenye gari na wakati huo kulikuwa na manyunyu ya mvua tukaendelea na safari na kufika Dodoma salama salimini.
Tazama namna Mama Tuma alivyonikaribisha na kunielekeza mengi juu ya biashara ya ndizi hadi namna ya kuzivundika. Mwanakwetu katika maisha ukisikia mtu amempenda fulani usiseme neno maana uzuri una mengi, kama ule wa Mke wa Mfalme Daudi(Abigaeli) kwani vipo vinavyoonekana kwa macho na visivyonekana.Ndani yake kuna urembo(namna mtu alivyo), akili(namna anavyofanya mambo yake) na utii(kwa wale wanaomtegemea).Je wewe uliyenaye anazo sifa hizo? Wewe mwenyewe unazo sifa hizo?
Mama Tuma wa Itewe anazo. Nakutakia siku njema.
makwadeladius@gmail.com
0717649257





0 Comments