Header Ads Widget

KATIBU MABIHYA AWACHARUKIA WATENDAJI WA SERIKALI KATIKA KUSIMAMIA MIRADI.



NA WILLIUM PAUL,  MOSHI. 

WATUMISHI wa umma wametakiwa kuwa macho katika kusimamia miradi mbalimbali inayoletwa na serikali ya Rais Samia Suluhu Hasani ili iweze kutimiza adhima iliyokusudiwa. 


Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM)  mkoa wa Kilimanjaro Jonathan Mabihya wakati wa ziara ya Wajumbe wa kamati ya Siasa mkoa kukagua miradi ya ujenzi wa madarasa 22 katika manispaa ya Moshi ikiwa ni fedha milioni 440 iliyotolewa na serikali ambazo ni  mradi wa mpango wa maendeleo endelevu na mapambano dhidi ya Uviko 19.




Katibu Mabihya alisema kuwa, Rais Samia anafikiria maslahi mapana kwa watanzania anaowaongoza hivyo ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha anamuunga mkono kwa kutimiza wajibu wake ili kuhakikisha anatimiza kile anachokikusudia. 


"Watumishi wa serikali mnapaswa kuwa macho katika miradi yote inayotekelezwa na Rais Samia kwani yeye mwenyewe hawezi kufika kila mradi na ndio maana mkawekwa kwa ajili ya kumsaidia kwa vitendo kuisimamia miradi hiyo" alisema Mabihya. 



Katibu huyo alisema kuwa,  thamani ya fedha ni lazima iendane na thamani ya mradi husika kwani kitendo cha miradi kukamilika lakini isidumu kutokana na kutokuwa bora sio jambo la kiungwana na halikubaliki. 


Alisema kuwa,  Rais Samia asingewaza jambo la ujenzi wa madarasa nchini mwakani hali ya uhaba wa madarasa ingekuwa mbaya na kupelekea wanafunzi wanaotarajiwa kuanza kidato cha kwanza kurundikana madarasani huku wengine kusubiria kwanza madarasa yajengwe. 



Kiongozi huyo alisema kuwa, jukumu la viongozi wa chama cha Mapinduzi ni kumsaidia Rais Samia kuhakikisha yale yote yaliyoahidiwa katika kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2020 yanatimizwa kwa vitendo. 


Aidha Katibu huyo alitumia nafasi hiyo kuwapongeza viongozi wa manispaa ya Moshi akiwamo Mkurugenzi kwa kusimamia vyema ujenzi wa madarasa hayo 22 huku akiwataka kuhakikisha kuwa changamoto ndogondogo zilizoainishwa katika baadhi ya majengo kufanyiwa kazi ndani ya siku saba ili yaweze kuendana na thamani ya fedha iliyotolewa. 



Kwa upande wake,  Mkurugenzi wa manispaa ya Moshi,  Rashidi Jembe alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Samia Suluhu Hasani kwa kuona umuhimu wa kutoa fedha za Uviko 19 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa.



Alisema kuwa, miaka ya nyuma wanafunzi wa kidato cha kwanza wanachelewa kuanza masomo kwa kusubiria kwanza ujenzi wa madarasa lakini kwa sasa madarasa yapo tayari yanawasubiria wanafunzi. 

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS