WIZARA ya Ujenzi na Uchukuzi wametiliana saini na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Nchini (TCAA) Mkataba wa usafiri wa anga kati ya Tanzania na nchi ya Ubelgiji. mwandishi wa matukio daima Hamida Ramadhan anaripoti kutokea Dodoma
Akizungumza leo jijini Dodoma Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa alisema Mkataba huo upo kisheria utawezesha nchi ya Tanzania na Ubelgiji kwa kutoa fursa kubwa kwa viwanja vya ndege vya Dar es Salaam, KIA na Zanzibar kupata fursa kubwa hasa ya wageni kuweza kuja moja kwa moja kutoka nchini ubelgiji mpaka Tanzania
Aidha alisema Mkataba huo utatoa fursa kwa shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kuweza kufanya safari za moja kwa moja kwenda huko Ubelgiji .
"Tunaamini Kabisa mkataba huu uliosainiwa leo utafungua milango mipya hasa kwa kupata watalii kutoka Ubelgiji na sehemu zingine huko duniani kwa sababu Ubelgiji ni nchi ambayo inauchumi mkubwa hivyo tunaamini mkataba huu utawezesha watalii wengi kuja kutembelea hapa Nchini Tanzania," Alisema Profesa Mbarawa
Aidha aliliomba shirika la ndege Tanzania ATCL kutambua kwamba milango imeshafunguliwa sasa wajipange waanze kufanya safari za ndege moja kwa moja kutoka Dar es Salaam mpaka nchini Ubelgiji.
Hata hivyo alitoa wito kwa watanzania kuchangamkia fursa hiyo kwa kuanza kufanya safari kupitia shirika la ndege la Air Tanzania na mashirika ya ndege Ubelgiji ili waweze kutembeleana na ndugu zao huko Ubelgiji
Kwa upande wake Balozi wa Ubelgiji hapa nchini Peter Van Acker alisema makubaliano hayo ni muhimu baina ya nchi ya Tanzania na Ubelgiji kwani kwasasa ndege za Tanzania zitaanza kufanya safari nchini Ubelgiji na Ndege za Ubelgiji kuanza safari kuja nchini Tanzania.
Pia alisema kupita makubaliano hayo viwanja vitatu vya ndege vitatumika kufanya safari hizo ambapo amevitaja viwanja hivyo kuwa ni kiwanja cha ndege cha jiji la Dar es Salaam, KIA na kiwanja cha ndege Zanzibar.
0 Comments