Header Ads Widget

WATAKIWA KUTUMIA MIKOPO YA HALMASHAURI KWENYE MALENGO YALIYOKUSUDIWA

Na,Jusline Marco ,Matukio Daima Arusha

Vikundi 50 vya wajasiriamali Halmashauri ya Arusha kwa makundi ya wanawake, vijana na wenye ulemavu wamekabidhiwa hundi ya shilingi Milioni 384  kama mkopo kutoka katika mapato ya ndani ya halmashauri hiyo ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Serikali.

Akikabidhi hundi hiyo Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhandisi Richard Ruyango ameupongeza uongozi wa halmashauri hiyo kwa utekelezaji wa vitendo ambapo amevitaka vikundi hivyo kuhakikisha vinatumia fedha hizo kwa malengo waliyokusudia na si vinginevyo kwani fedha hizo ni za jamii  nzima na maendeleo yao kwa ujumla.



"Mikopo hii ya asilimia 10 ya mapato ya ndani inatokana na kodi zenu zinazokusanywa na halmashauri yenu kupitia vyanzo mbalimbali vya mapato, hivyo serikali ya awamu ya sita ikaona ni vyema kurudisha asilimia 10 ya mapato yake kwa wananchi kwa kuwapa mikopo isiyokuwa na riba, ili wananchi waweze kunufaika na itakayozalisha faida kwa kuongeza kipato cha familia na taifa kwa ujumla."alisema Mhandisi Ruyango


Aidha kutokana na idadi ndogo ya vijana waliojitokeza katika vikundi hivyo na kujitokeza kutumia fursa hiyo ukilinganisha na vikundi 40 vya wanawake vilivyojitokeza kuomba mikopo hiyo kumesababisha uzorotaji wa maendeleo ya vijana nchini, vijana mbao taifa linawategemea.


"Katika shilingi milioni 384, vijana wanapata milioni 85 tu, niwasihi vijana wangu tumieni fursa hii kwa kuchukua hatua ya kujiunga kwenye vikundi ili kupata mikopo hii na anzisheni biashara ndogo ndogo kupitia raslimali zinazopatikana katika maeneo yenu, msisubiri kuajiriwa tu!" amesistiza Mkuu huyo wa Wilaya.


Kutokana na hilo Mhandisi Ruyango ameiagiza Idara ya Maendeleo ya Jamii kuendelea kutoa elimu kwa vijana na kuwafikia vijana wengi zaidi katika maeneo yao ili wapate uelewa juu ya mikopo hiyo na kujiunga kwenye vikundi vitakavyowawezesha kutumia fursa hii ya kupata mikopo isiyo na riba inayotolewa na serikali yao.



Naye Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Suleman Msumi katika makabidhiano hayo amesema kuwa halmashauri hiyo imetimiza wajibu wao wa kutenga asilimia kumi  katika makundi hayo hivyo watumize wajibu kuzirejesha ili wengine waweze kupata fedha  hizo.


"Katika mapato ya halmashauri kwa kipindi cha miezi mitatu ya robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2021/2022, halmashauri imetenga jumla ya shilingi milioni 384 ikiwa ni asilimia 10 ya fedha zilizokusanywa, kwa ajili ya kutoa mikopo isiyokuwa na riba kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu."alisema Msumi


Amebainisha kuwa kiasi hicho cha fedha kimetolewa kwa vikundi 40 vya wanawake vilivyokopeshwa shilingi milioni 325.5, vikundi 10 vya vijana vilivyokopeshwa shilingi milioni 48,na watu wawili wenye ulemavu waliokopeshwa shilingi milioni 10.5 na kufanya jumla ya shilingi milioni 384.


"Haya ni mafanikio na katika matimizo ya nia nzuri ya Mhe.Rais Samia Suluhu katika kuhakikisha kwamba kila mtanzania anatoka katika hali ya umaskini,kama mnavyoelewa huwezi ukafanya biashara bila kuwa na mtaji kwa maana hiyo kwamba mkopo ni mtaji ili uweze kuweza kufanyabiashara na kujiongezea kipato hivyo katika kuliona hilo tumetenga kiasi hicho cha fedha.


Vilevile amesema zoezi hilo limeenda kwa mafanikio makubwa kwani wamefanikiwa kuhamasisha jamii ili mikopo iweze kufikia watu wengi zaidi na kuahaidi kuwa halmashauri hiyo itaendelea kutenga fedha hizo kama walivyohimizwa na serikali ili ziweze kuwasaidia wajasiramali katika kujikwamua kiuchumi.


"Zoezi hili pia limeonyesha mafanikio kwa kuzalisha ajira kupitia vikundi hivyo ambapo kipato cha mtu mmoja mmoja kinaweza kukua kupitia uanachama wa vikundi hivyo sambamba na halmashauri kupata mafanikio kwa kufungua akaunti ambayo itatumika katika kuweka marejesho hayo "Alisema Mkurugenzi huyo


Sambamba na hayo Msumi amewataka wanufaika hao kutohusisha mikopo hiyo yenye lengo la kufanya shughuli za kujikwamua kiuchumi kwa kuzielekeza katika shughuli za kibinafsi na kutunza familia bali watambue kuwa dawa ya deni ni kulipa hivyo wanapaswa kuwa makini ili wasiweze kukuza mitaji yao na kuwezesha wengine kunufaika.


Mmoja Elibariki Munga ambaye ni fundi wa kushona sare za shule kupitia kundi la watu mwenye ulemavu akitoa shuktani baada ya kupokea mkopo huo ameahidi kuwa mwaminifu katika kurejesha fedha hizo huku akisistiza wanakikundi wengine kurejesha kwa uaminifu fedha walizopokea na kuishukuru serikali kwa kuthamini kundi la watu wenye ulemavu tofauti na hapo awali.


"Tutakuwa waminifu katika kurejesha mikopo hii ni naamini kati ya watu ambao watakuwa waaminifu kurejesha fedha hizo ni sisi watu wenye ulema naahidi kurejesha fedha hizi kwa wakati bila usumbufu wowote" amethibitisha Munga.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Arusha, Mhe.Ojung'u Salekwa amewasihi wanavikundi hao hasa kina mama kuwa makini na miezi hii ya sherehe kwa kuacha kushawishika kutumia fedha hizo kwenye sherehe zinazofanyika kila mwisho wa mwaka.


"Mmepokea fedha hizi, kipindi ambacho kuna sherehe nyingi za kufunga mwaka, msije mkatumia fedha hizo kwenye ubarikio, 'mbesii' za kina mama, wala kununua vitenge vya 'wax' doti 60 kwa ajili ya 'send off', tumieni fedha hizo kuzalisha na kujionhezea kipato cha familia pamoja na kurejesha kwa wakati" amesisitiza Mwenyekiti huyu wa Halmashauri.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI